Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu

(DSFA)

Mhe. Silinde aongoza mapokezi ya tani 25.8 za samaki wasiolengwa

Imewekwa: 17 September, 2023
Mhe. Silinde aongoza mapokezi ya tani 25.8 za samaki wasiolengwa

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ameongoza mapokezi ya tani 25.8 ya samaki wasiolengwa au "bycatch" kama inavyojulikana kitaalam ambao wamevuliwa katika ukanda wa bahari kuu.

Katika hafla ya mapokezi ya samaki hao wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 85 za kitanzania iliyofanyika Wilaya ya Mwanakwerekwe visiwani Zanzibar Mhe. Silinde ameipongeza kampuni ya "Albacora" inayomiliki meli ya "Pasific Star" kwa kuanza kutekeleza sehemu ya makubaliano baina yake na mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambapo Meli hiyo itakuwa ikishusha kiasi cha tani 100 za samaki wasiolengwa kila mwaka.

"Samaki hawa tulioanza kuwapokea leo wataongeza mapato ya Serikali kupitia chanzo hiki kipya, usalama wa chakula na lishe na kutokana na wingi wa samaki watakaokuwa wakishushwa nina uhakika hata bei ya samaki hapa nchini itapungua na hivyo kuwawezesha wananchi wengi hususan wenye kipato cha chini kumudu gharama za bidhaa hii" Amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde ameongeza kuwa hatua hiyo pia itaimarisha biashara ya samaki hasa kwa wanawake ambao wamekuwa wakijihusisha na ununuzi na uuzaji wa samaki nchini na hivyo kuboreshw mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo kwa ujumla.

"Serikali inayoongozwa na mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada nyingi sana katika kuimarisha sekta ya Uvuvi na kuongeza mapato yatokanayo na sekta hiyo kwa ujumla hivyo tunategemea uvuvi wa bahari kuu utakuwa ni moja ya chanzo kikubwa sana cha mapato nchini " Amesisitiza Mhe. Silinde.

Aidha Mhe. Silinde ameipongeza kampuni ya Albacora kwa kuanza utekelezaji wa makubaliano yake na Mamlaka ya wa bahari kuu ambapo amesema kuwa Serikali inataka wawekezaji wa aina hiyo na hivyo kuiomba Mamlaka hiyo kuendelea na jitihada za kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Meli ya "Pasific Star" inayomilikiwa na kampuni ya Albacora imepewa kibali cha kuvua samaki katika ukanda wa bahari kuu ikiwa ni moja ya hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza dhana kwa vitendo dhana ya uchumi wa buluu.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo