WATUMISHI WAPYA WA MAMLAKA WAPEWA MAFUNZO YA AWALI
Waajiriwa Wapya na Watumishi waliohamia katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wapewa mafunzo ya awali kazini kwa lengo la kuwakaribisha rasmi kujiunga na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), pamoja na kuwasaidia kupata uelewa wa Sheria, Taratibu, Kanuni na Misingi ya Utumishi ili kutimiza malengo ya Serikali.
Mafunzo hayo yametolewa kwa watumishi wapya 25, Disemba 11, 2023 katika ukumbi wa Bunge jijini Dar es Salaam ambapo mada mbalimbali ziliweza kuwasilisha na viongozi kutoka Mamlaka zikiwemo majukumu ya Kurugenzi zilizopo, Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma pamoja na kufahamu umuhimu wa huduma kwa wateja, mawasiliano ya kiofisi na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa Mamlaka imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya awali kwa Watumishi wote wanaojiunga na Mamlaka kwa njia ya ajira mpya au uhamisho kwa lengo la kuwafahamisha majukumu na utamaduni wa taasisi, hivyo, amewataka watumishi wapya kuwa watiifu kwa kufanya kazi kwa kuheshimu kanuni za Utumishi wa umma na weledi ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya taasisi.
“Mamlaka inatoa mafunzo haya kwa lengo la kuhakikisha Watumishi wote wa Mamlaka wanaelewa vema majukumu ya Mamlaka na utamaduni wake, hivyo kuwezesha utekelezaji wa majukumu wenye ufanisi zaidi kwa kuwa taasisi hii ni miongoni mwa taasisi muhimu za Umma ambayo inahitaji watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu,” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kuijua vyema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa maana ya majukumu yake ya msingi kwa Serikali na Jamii ya Watanzania na kujifunza umuhimu wa utunzaji wa siri ambao ni moyo wa utendaji wa Mamlaka.
Dkt. Mafumiko amewasihi washiriki hao wa mafunzo kuwa wasikivu katika kipindi chote cha mafunzo na pia wasisite kuuliza maswali pale inapolazimu ili waweze kutoka wakiwa wameelewa namna shughuli zinavyofanyika katika taasisi na namna ya kuenenda katika kipindi chote watakapokuwa watumishi wa Mamlaka.
