Tanzania emblem

Blogu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

NAIBU WAKILI MKUU WA SERIKALI AFUNGUA MAFUNZO YA UADILIFU

NAIBU WAKILI MKUU WA SERIKALI AFUNGUA MAFUNZO YA UADILIFU
22nd Nov 2024

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo amefungua mafunzo kwa Kamati ya Uadilifu na kwa Menejimenti Maalum ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 20 Novemba, 2024 hadi tarehe 23 Novemba, 2024.

Bi. Mtulo amefungua mafunzo hayo ili kujenga uelewa kwa Kamati ya Uadilifu ya OWMS na kwa wajumbe hao ili wafahamu majukumu yao na kujipanga kuyatekeleza kwa kuzingatia matakwa ya Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne (NASCAP- 2023/2030). Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeunda Kamati ya Uadilifu kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298 kama ilivyorejewa 2019 pamoja na Waraka uliotolewa na Serikali wa kuzitaka Ofisi za umma kuanzisha Kamati za Maadili ambapo OWMS imemteua Bi. Vivian Method kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uadilifu wa Ofisi hiyo.

Bi. Mtulo aliongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia uelewa wajumbe wa Kamati kuhusu malengo ya kamati, wajibu wa wajumbe wa Kamati, namna Kamati zinavyotekeleza majukumu yake pamoja na kuelewa mategemeo ya Serikali kwa Kamati.

‘’Mafunzo haya tuyachukulie kwa uzito wake na kwa umakini kwa kuwa hayatusaidii tu kwenye Ofisi bali hata kwenye maisha yetu nje ya Ofisi ili kujenga jamii inayoishi na kuzingatia maadili,’’ amesisitiza Bi. Mtulo.

Pia, ametoa rai kwa washiriki kutumia fursa hiyo adhimu kupata mafunzo hayo na kwenda kufanyia kazi ipasavyo yale yote watakayofundishwa ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa manufaa ya Taifa na wananchi kwa ujumla. Mafunzo hayo yametolewa na wataalam wa Ofisi ya Rais Ikulu.

Maoni