BMH YAANZISHA HUDUMA ZA KUPANDIKIZA BETRI KWENYE MOYO
Published on August 12, 2022
BMH yaanza kupandikiza betri kwenye moyo
Na Ludovick Kazoka
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) kupitia Idara yake ya Matibabu ya Magonjwa ya Moyo imeanza kupandikiza betri kwenye moyo kwa watu wenye tatizo la mapigo ya moyo ya chini 40 yanayoambatana na dalili
Upandikizaji wa betri kwenye moyo ni upandikizaji wa kifaa cha kieletroniki kwenye moyo kwa watu wenye tatizo la mapigo ya moyo ya chini. Upandikizaji wa betri kwenye moyo upo wa aina mbili wa kudumu na usio wa kudumu.
Mkuu wa Idara ya Matibabu ya Magonjwa ya Moyo, Dkt Happiness Kusima, ameliambia jarida hili kuwa mapigo ya moyo ya kawaida ni kuanzia 60 mpaka 100 kwa mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 12 na wengi wanaohitaji upandikizaji huo ni walio na mapigo chini ya 40 yanayoambatana na dalili.
“Mpaka sasa, tumepandikiza betri kwa watu wawili waliokuwa na tatizo la mapigo ya moyo ya chini, mmoja tulimpandikiza tarehe 1 na wa pili tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka huu 2021” alisema Mkuu wa Idara ya Matibabu ya Moyo katika BMH.
Watu gani wanapandikizwa betri kwenye moyo
Kwa mujibu wa Dkt Kusima, watu wenye mapigo ya moyo chini ya kiwango cha 40 yanayoambatana na dalili wanapandikizwa betri kwenye moyo baada ya kupitia vipimo kadhaa vya moyo
Pia, anasema kuwa baadhi ya watu wenye tatizo la kushindwa kwa moyo (heart failure) ambao baada ya uchunguzi kuonekana wana hitilafu kwenye mfumo wa umeme wanapandikizwa betri kwenye moyo.
Bi. Heavenlight Massawe, alieyepandikizwa betri ya moyo hospitalini BMH, anasema sasa hivi mapigo yake ya moyo yanaenda sawa, akiongeza kuwa hata akitembea haemi kama ilivyokuwa kabla hajapandikizwa betri ya moyo.
“Nawashukuru sana Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa huduma nzuri. Tatizo lililonisumbua kwa muda wa miaka saba iliyopita, sasa limeisha,” anasema Bi Massawe, ambaye ni mkazi wa Arusha.
Mzee Henri Kiwaya, aliyepandikizwa betri ya moyo Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), anasema sasa anaweza kufanya shughuli zake kawaida bila kuhema sana kama ilivyokuwa awali, anasema alikuwa akipanda ngazi akifika anapoenda inabidi apumpumzike kwanza kutokana na ‘kuishiwa pumzi’.
“Huduma zenu ni nzuri. Watumishi wenu ni wakarimu sana. Sasa, sijambo tatizo lililonisumbua kwa muda wa zaidi ya mwaka, sasa limeisha,” Mzee Kiwaya, ambaye ni mkazi wa Dodoma, alimwambia mwandishi wa makala haya.
Dalili za watu wenye tatizo la mapigo ya moyo chini ya kiwango cha 40
- Uchovu wa hali ya juu
- Kupoteza fahamu
- kupata shida ya kupumua.
- Kizunguzungu
- Maumivu kwenye kifua
Hata hivyo, Dkt Kusima, anasema sio kila mtu mwenye mapigo chini ya kiwango cha 40 anapaswa kupandikizwa betri kwenye moyo, akisema mapigo ya moyo chini ya 40 ndiyo yakiambatana na dalili hizo ndiyo anafanyiwa vipimo kuangalia uwezekano wa kumpandikizia betri.
VIPIMO
Madaktari pia watachukua historia ya mgonjwa ili kubaini magonjwa na matibabu aliyopata kipindi cha nyuma ikiwepo dalili alizokuwa nazo.
Mgonjwa hufanyiwa vipimo kadha wa kadha vya maabara,kubanini sababu au vitu vinavyoongeza tatizo la kuwa na mapigo chini ya kiwango.
Vipimo vya moyo
Vipimo vingine anavyopitia mtu mwenye mapigo ya chini ya kiwango cha 40 zinazoambatana na dalili ni Holter ECG pamoja na Stress ECG. Vipimo vyote hivi vinapatikana Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma
CHANZO
Umri unaweza kuwa mojawapo ya chanzo cha mapigo kuwa chini ya kiwango cha 40. Wazee wanaweza kupata tatizo hili
Baadhi ya maradhi ya moyo yanaweza kuwa sababu ya mapigo ya moyo kuwa chini ya kiwango cha 40
Matibabu yanayotumika kutibu shinikizo juu la damu na magonjwa mengine ya moyo ikiwemo ya mfumo wa umeme.( DAWA)
Upasuaji wa moyo unaweza kuwa sababu ya mapigo ya moyo chini ya kiwango cha 40,upasuaji huweza kuathiri mfumo wa umeme
BAADA YA KUPANDIKIZWA BETRI
Baada ya kupandikizwa betri kwenye moyo, mtu atapaswa aishi maisha ya tahadhari ikiwa ni pamoja na matumizi ya simu.
Mtu atapaswa aiweke mbali kama nchi sita anapo pokea simu ili kuepusha mawimbi kuhitalifiana na betri aliyopandikizwa.
Mwenye betri kwenye moyo pia hatopaswa kupita kwenye ving’amuzi chuma (metal detectors) sababu inaweza kuhitalifiana na betri hilo.
Atapaswa kuepuka matumizi ya sigara za kielectroniki (e-cigarette) na mazoezi ya nguvu. Pia aepuke vifaa vya umeme ambavyo vina hitilafu kama micro wave na blanketi ya kielectroniki.
UMRI WA BETRI
Baada ya kupandikizwa betri, mtu anaweza kudumu na betri moyoni kwa muda wa muda wa miaka sita mpaka kumi na mbili kabla ya haijabilishwa tena.
Mtaalamu wa Mishipa ya Moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Godfrey Temba, akiangalia mapigo ya moyo kwenye kifaaa maalumu kinanchoitwa kitaalamu pacemaker programmer and monitoring device katika Maabara Maalumu ya Moyo (Catheterization laboratory) ya BMH.