Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Pamba Tanzania

WADAU WA PAMBA WAPONGEZA MRADI WA BBT - PAMBA

Imewekwa: 27 August, 2025
WADAU WA PAMBA WAPONGEZA MRADI WA BBT - PAMBA

WADAU WA PAMBA WAPONGEZA MRADI WA BBT - PAMBA

Wadau wa Pamba wameipongeza serikali kwa kuanzisha Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), jambo ambalo limeleta nidhamu katika sekta ya Pamba ikiwemo kuongeza uzalishaji, kudhibiti ubora na kusimamia upatikanaji wa takwimu sahihi za Pamba na wakulima. 

Aidha, wadau hao pia wameipongeza Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Pamba kwa kuanza maandalizi mapema ya msimu wa Kilimo 2025/26 kwa kuandaa mbegu ili ziwafikie wakulima kwa wakati.

Akizungumza hivi karibuni ofisini kwake, Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa kiwanda cha Alliance Ginneries Ltd kilichopo Bariadi mkoani Simiyu Bw. Boaz Ogolla amesema kuwa hadi mwishoni mwa wiki jana (August 17, 2025) wamenunua zaidi ya kilo Mil. 138 tofauti na mwaka jana, muda kama huo.

Ogolla ameipongeza serikali kwa kuja na mpango wa Maafisa ugani kupitia Mradi wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT) kwa usimamizi mzuri wa zao hilo ambapo kuna viashiria vya kuongezeka kwa ubora kwa 40% kwa madaraja ya Gany za Zaidi limeongeza tofauti na msimu uliotangulia kwa mujibu wa taarifa maabara ya usanifu wa ubora wa madaraja ya pamba.

"Ubora wa Pamba wa mwaka huu umeongozeka, ukilinganisha na Ubora wa mwaka jana, taarifa ya Maabara kutoka Bodi ya Pamba imebadilika...BBT wameisaidia sana kusimamia na kudhibiti uchafuzi wa Pamba,.pia tumepata takwimu halisi za wakulima na mashamba yao" Amesema.

Ogolla ambaye pia ameiomba serikali kupeleka Maafisa Ugani wa BBT kwenye kata ambazo hazikuwa na wataalamu hao ili waweze kuwasimamia wakulima katika msimu ujao.

Kuhusu viongozi wa Amcos kuchezea mizani, Ogolla aliiomba serikali kuwachukulia hatua kali ambao wamebainika kuchezea mizani ya pamba kwa lengo la kuwainia wakulima wa Pamba jambo ambalo ni tofauti na malengo ya Amcos kusimamia maslahi ya wakulima.

Kwa upande wao wakulima wa Pamba wameipongeza serikali kusimamia sekta ya Pamba kupitia Maafisa Ugani wa BBT ambao wameonyesha tija na mabadiliko ya uzalishaji.

Masunga Liki, mkazi wa Kijiji cha Nyanguge amesema kuwa Mpango huo umewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kutoka kilo 200 mpaka 300 walizokuwa wanazalisha kwa ekari moja na kufikia kilo 600 mpaka 800 kwa ekari.

Ameongeza kuwa wakulima hao wameona mabadiliko katika sekta ya Pamba na kushauri Elimu ya ugani, matumizi sahihi ya mbolea na Pembejeo yazingatiwe ili wakulima waongeze tija.

Naye Kundi Mashini, mkulima wa Pamba Kijiji cha Mhunze wilayani Itilima, ameiomba serikali kuwafikishia Matrekta ya serikali kwa wakati ili waweze kulima mapema wakiendana na kalenda ya Kilimo cha pamba.