Historia
Historia ya Bodi ya Pamba inaenda sanjari na maendeleo ya zao la pamba hapa nchini. Pamba iliingizwa nchini Tanganyika na wakoloni wa Kijerumani mnamo mwaka 1903, lakini uzalishaji wa pamba kibiashara ulianza mwaka 1922 wakati huo Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa wakoloni Waingereza. Pamba ilianza kuzalisha katika mikoa ya Kanda ya Mashariki ambayo inajumuisha Morogoro, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Iringa na Mbeya. Aidha kwa sasa mkoa wa Mbeya uko chini ya Karantini kutokana na kuwepo kwa mdudu aitwaye funza mwekundu mweupe ambaye bado njia za kumdhibiti hazijapatikana.
Miaka michache baadaye zao la pamba lilienezwa katika mikoa ya Kanda ya Magharibi wakati huo ikijulikana kama Usukumani. Kanda ya Magharibi inajumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Kagera na Kigoma. Hadi kufikia mwaka 1930 uzalishaji wa pamba ulishafikia zaidi ya marobota 7,200, marobota 4,000 yalizalishwa katika Kanda ya Mashariki na marobota 3,200 katika Kanda ya Magharibi.
Kutokana na sera za Kikoloni za kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vilivyokuwa katika mataifa yao pamba yote iliyozalishwa nchini Tanganyika ilikuwa inasafirishwa nje ya nchi. Kwa kuwa hapakuwepo na chombo cha kusimamia usafirishaji wa pamba nje, serikali ya Kiingereza ilisafirisha pamba kupitia kampuni ya Victoria Federation iliyokuwa na makao makuu nchini Uganda. Kutokana na hali hii serikali ya kikoloni ililazimika kuunda chombo cha usimamizi wa shughuli za pamba. Bodi ya Pamba ya kwanza iliyojulikana kama Lint and Seed Marketing Board of Tanganyika iliundwa mwaka 1952 chini ya sheria “Lint and Seed Marketing Ordinance” ya mwaka 1952. Majukumu makuu ya Bodi yalikuwa kusimamia uzalishaji na uuzaji wa pamba ya Tanganyika. Chini ya LSMBT uzalishaji wa pamba uliongezeka kwa kasi na ilipofika mwaka 1959 uzalishaji ulifikia marobota 184,000.
Baada ya Uhuru
Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, LSMB iliendelea kusimamia majukumu ya kuendeleza zao la pamba hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo na ulipofika mwaka 1966 mwaka mmoja kabla ya Azimio la Arusha uzalishaji wa pamba ulifikia marobota 440,000. Baada ya Azimio la Arusha Bodi ya Pamba ilipunguziwa majukumu na ilibaki jukumu la kusimamia maendeleo ya zao la pamba na shughuli za ununuzi kufanywa na Vyama vya Ushirika.
Aidha mwaka 1973, Bodi ya Pamba Tanganyika ilifutwa na kuanzishwa Mamlaka ya Pamba Tanzania chini ya sheria namba tatu ya mwaka 1973 -Cotton Authority Act. Mamlaka ya Pamba ilikuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya sekta ya pamba ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za ugani na kusambaza pembejeo kwa wakulima kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika.
Mabadiliko ya kisera ya mwaka 1976 yalivifuta Vyama vya Ushirika nchini na majukumu yote ya kusimamia zao la pamba kuanzia uzalishaji, ununuzi, uchambuaji na mauzo ya pamba nje ya nchini kufanya na Mamlaka ya Pamba Tanzania. Aidha mwaka 1984, Serikali ilirejesha Vyama vya Ushirka na kuvipa jukumu la kununua pamba kutoka kwa wakulima na kuchambua. Kutokana na mabadiliko haya Serikali iliifuta Mamlaka ya Pamba na kuanzisha Bodi ya Pamba (Tanzania Cotton Marketing Board) chini ya sheria namba 19 ya mwaka 1984. Bodi ya Pamba ilipewa majukumu ya kununua pamba nyuzi kutoka Vyama vya Ushirika na kuuza nje ya nchi na kuagiza pembejeo za pamba ambazo zilisambazwa kwa wakulima kwa mkopo na Vyama vya Uushirika.
Sheria namba 19 ya mwaka 1984 iliyounda TCMB ilifanyiwa marekebisho na miscelleneous Act No. 11 ya mwaka 1991 ambapo baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vilivyokuwa vinataja jina la TCMB vilifutwa na kuwa TCL&SB na majukumu ya Bodi hii kuwa ya usimamizi wa sheria na kanuni za pamba pamoja na uwakala kwa Vyama vya Ushirika. Bodi ilikuwa inauza Pamba kwa niaba ya Vyama vya Ushirika. Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilianzisha sera ya ubinafsishaji na soko huru katika sekta zote ikiwa ni pamoja na sekta ndogo ya pamba mwaka 1993. Ili kuwezesha Bodi kwenda na sera ya soko huru, sheria namba 19 ya mwaka 1984 ilifanyiwa marekebisho tena kwa “miscellenous Act No.13 of 1993” ambayo ilifuta majukumu yote ya kibiashara na kuifanya Bodi ya Pamba kuwa chombo cha usimamizi sera na sheria za Pamba kwa niaba ya Serikali.
Wakati Bodi (TCMB) inapewa jukumu la kununua pamba toka Vyama vya Ushirika na kuuza nje ya nchi, uzalishaji wa pamba ulikuwa tani za pamba mbegu 155,115 sawa na marobota 287,250 ya pamba nyuzi, lakini kutokana na usimamizi mzuri katika upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, uzalishaji uliendelea kuongezeka japokuwa katika misimu mingine uzalishaji ulishuka kutokana na hali mbaya ya hewa. Mwaka mmoja kabla ya kuanza kwa sera ya soko huru uzalishaji wa pamba ulifikia tani za pamba mbegu 308,265 sawa na marobota 570,861 katika msimu wa 1992/93 ukiwa ni uzalishaji mkubwa kuwahi kufikiwa tangu uzalishaji mkubwa ulipofikiwa mwaka 1966 ambapo marobota 440,000 yalizalishwa..
Sekta Ndogo ya Pamba Baada ya Soko Huru.
Mwanzoni mwa miaka 1990 Serikali ya Tanzania ilianzisha sera ya soko huru katika sekta zote ikiwemo sekta ndogo ya pamba. Sera ya soko huru ilianzishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi hasa katika sekta zote za kibiashara. Soko huru katika zao la pamba lilikuwa na maendeleo chanya na hasi. Maendeleo chanya ya soko huru katika zao la pamba ni pamoja na;
- Kuongezeka kwa ushindani katika ununuzi wa pamba. Idadi ya wanunuzi wa pamba iliongezeka hali ambayo ilileta ushindani na kufanya pamba ya wakulima inunuliwe kwa wakati.
- Wakulima kulipwa bei nzuri kwa wakati bila kukopwa. Wakulima walianza kulipwa bei nzuri kwa pamba yao iliyolingana na hali halisi katika soko la dunia na bila kukopwa. Asilimia ya bei aliyokuwa anayolipwa mkulima imeongezeka kutoka asilimia 28 kabla ya soko huru hadi kufikia 60 na zaidi kwa sasa.
- Kuongezeka kwa ufanisi katika uchambuaji wa pamba. Idadi ya viwanda vya kuchambua pamba viliongezeka kutoka viwanda 37 vilivyokuwepo kabla ya soko huru hadi kufikia viwanda takriban 80 sasa.
Maendeleo hasi ya sera ya soko huru ni pamoja na;
- Kushuka kwa usafi na ubora wa pamba. Kutokana na kutokuwepo kwa ushindani wa haki wanunuzi walianza kununua pamba bila kuzingatia kanuni za usafi na ubora wa pamba hasa kununua pamba ambayo haikutengwa katika madaraja ya A na B. Pamba ya Tanzania imepoteza sifa katika soko la kimataifa kutokana na kuongezeka kwa uchafu.
- Kushuka kwa tija na uzalishaji wa pamba. Kutokana na kutokuwepo kwa mfumo unaoeleweka chini ya soko huru unaolekeza nani mwenye jukumu la kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima na utoaji wa elimu ya ugani kwa wakulima, uzalishaji wa pamba ulishuka kwa kiwango kikubwa kutokana na wakulima kukosa mbegu, madawa na huduma za ugani. Wafanyabiashara walilenga katika kununua pamba tu bila kujali kuwa mkulima alihitaji mbegu na madawa.
- Kusambaratika kwa mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo. Kabla ya soko huru pembejeo zilikuwa zinaagizwa na Bodi ya Pamba na kusambazwa na Vyama vya Ushirika kwa mkopo. Wakulima walilipa madeni ya pembejeo wakati wa kuuza pamba. Ujio wa soko huru ulilenga zaidi ununuzi wa pamba lakini suala la upatikanaji wa pembejeo halikupewa nafasi. Kutokana na kukosekana kwa pembejeo uzalishaji ulishuka kutoka tani 308,265 kabla ya soko huru hadi tani 100,560 za pamba mbegu msimu wa 1999/2000.
- Kusambaratika kwa mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba. Baada ya soko huru suala la nani asimamie uzalishaji wa mbegu za kupanda halikupewa kipaumbele. Ununuzi wa pamba kwa kuzingatia kanda kama ilivyokuwa inafanywa na Vyama vya Ushirika haukuzingatiwa hali ambayo ilisababisha kuchanganyika kwa mbegu za UK 77 na UK82. Aidha utafiti wa mbegu bora ambayo ingechukua nafasi ya mbegu za awali ulisitishwa kutokana na kukosekana kwa fedha.
- Kukosekana kwa wanunuzi katika Kanda ya Mashariki na maeneo mengine ya Kanda ya Magharibi yenye uzalishaji mdogo. Soko huru linalenga zaidi kupata faida na siyo kutoa huduma, na kwa hali hii mikoa ya Kanda ya Mashariki ambayo uzalishaji wake ni mdogo sana yalikosa soko hivyo wakulima kukata tamaa ya kuendelea kuzalisha pamba.
Pamoja na kwamba kushuka kwa uzalishaji kulichangiwa na sera ya soko huru lakini zipo sababu zingine zilizochangia kushuka kwa uzalishaji, tija na ubora wa pamba ambazo ni pamoja na;
- Wakulima kutokuzingatia kanuni kumi za kilimo bora cha pamba hasa kupanda pamba kwa mistari na nafasi inayopendekezwa na matumizi ya mbolea ya samadi. Wakulima wameendelea kupanda pamba kwa kusia na kuchanganya pamba na mazao mengine hali ambayo inafanya kuwa na mimea michache sana kwa eneo. Aidha mbolea ya samadi inapatikana kwa gharama kidogo kwa urahisi lakini wakulima hawaoni umuhimu wa kuweka mashambani.
- Mabadiliko ya mara kwa mara ya hali ya hewa. Pamba nchini Tanzania inazalishwa kwa kutegemea mvua kwa asilimia 100 na ambazo si za uhakika. Mvua zinapokuwa za kutosha uzalishaji unaongezeka na kunapotokea ukame uzalishaji unashuka.
- Mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya pamba. Bei imekuwa kichecheo kikubwa sana cha wakulima kuzalisha pamba. Bei ikiwa nzuri msimu huu pamba inazalishwa kwa wingi sana msimu unaofuata. Aidha bei inaposhuka wakulima wengi wanaacha kuzalisha pamba na kuzalisha mazao mengine.
Mikakati ya kuboresha sekta ndogo ya pamba.
Mikakati mbalimbali imebuniwa na Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na wadau wa zao la pamba kwa lengo la kutatua matatizo ya msingi yanayokwamisha zao la pamba hapa nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na;
1. Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Pamba
Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na wanunuzi wa pamba walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1999 kujadili suala la kushuka kwa uzalishaji, ubora wa pamba na upatikanaji wa pembejeo na kuamua kuanzishwa kwa Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba ambao ulikuwa na majukumu ya msingi ya kuhakikisha upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, kufadhili shughuli za utafiti wa mbegu bora na kuandaa na kutoa taarifa kwa wadau.
2. Agizo la Mwanza la Mwaka 2000
Mkutano wa wadau wa zao la pamba uliokaa jijini Mwanza mwaka 2000 ulipitisha Agizo la Mwanza la kuboresha Sekta Ndogo ya Pamba pamoja na Mkakati wa Kuendeleza Zao la Pamba. Agizo la Mwanza lilichambua kwa kina sababu zinazokwamisha maendeleo ya Sekta Ndogo ya Pamba na kubuni mikakati ya kuitatua. Mikakati hiyo ilitekelezwa katika Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya pamba iliokuwa na lengo la kuongeza Uzalishaji wa Pamba hadi kufikia marobota laki saba (700,000) ufikapo msimu wa 2005/06, lengo ambalo lililifikiwa kama ilivyokusudiwa.
3. Mpango wa Kitaifa wa Pembejeo za Pamba.
Baada ya kubaini kwamba upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima hautoshi kama wakulima hawana uwezo wa kununua pembejeo hizo, Bodi ilibuni Mpango wa Kitaifa wa Pembejeo za Pamba “Passbook” mwaka 2004 ambapo mkulima alikuwa anajiwekea akiba ya kununulia pembejeo za pamba msimu ujao wa kilimo wakati wa kuuza pamba yake. Mpango huu ulionesha mafanikio makubwa sana na uzalishaji uliweza kuongezeka hadi kufikia uzalishaji wa kihistoria wa tani 376,591 za pamba mbegu katika msimu wa 2005/06. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wa Bodi, Mpango wa Pembejeo ulifutwa katika msimu wa 2006/07.
4.Kutungwa sheria ya pamba Na 2 ya mwaka 2001
5.Kilimo cha Pamba cha Mkataba
Kufutwa kwa Mpango wa Kitaifa wa Pembejeo za pamba “Passbook” kumesababisha wakulima wengi kushindwa kumudu kununua pembejeo kwa fedha taslimu, hivyo uzalishaji ulianza tena kushuka. Kukabiliana na tatizo la kushuka kwa uzalishaji, Bodi ilibuni utaratibu mwingine ambao ni endelevu utakaomwezesha mkulima kupata huduma mbalimbali kwa uhakika. Bodi ya Pamba kwa kusihikiana na Tanzania Gatsby Trust, ilianzisha kilimo cha mkataba kwa majaribio katika mkoa wa Mara kuanzia msimu wa 2008/09 na ukaonesha mafanikio makubwa. Kutokana na mafanikio yaliyopatikana, msimu huu wa kilimo wilaya ya Bariadi ilijumuishwa katika utaratibu wa kilimo cha mkataba katika msimu wa kilimo wa 2010/11. Ili kuwezesha utaratibu huu kutekelezwa nchi nzima, Sheria ya Pamba Na 2 ya mwaka 2001 ilifanyiwa marekebisho ili kuipa Bodi uwezo wa kusimamia kilimo cha mkataba. Utaratibu huu ambao utamlazimu mnunuzi wa pamba kuingia mkataba na mkulima kwa kumpatia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na pembejeo na huduma za ugani na mwisho kununua pamba kutoka kwa mkulima umeenezwa katika mikoa yote inayozalisha pamba Kanda ya Magharibi katika msimu wa kilimo wa 20011/12