Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Pamba Tanzania

UKAGUZI KWA KUTUMIA VIPIMO VYA KISASA KUIMARISHA USAFI NA UBORA WA PAMBA

Imewekwa: 27 August, 2025
UKAGUZI KWA KUTUMIA VIPIMO VYA KISASA KUIMARISHA USAFI NA UBORA WA PAMBA

Bodi ya Pamba Tanzania imeendelea kutoa elimu kwa wakulima wa pamba huku ikitambulisha matumizi ya mashine maalum ya kupima unyevunyevu kwenye pamba (Cotton Moisture Meter), kwa lengo la kulinda ubora wa zao hilo muhimu la kibiashara na kudhibitiuchafuzi unaofanywa kwa kuchanganya maji

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha sekta ya pamba, kuhakikisha uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani ya pamba ya Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkaguzi wa Pamba wilayani Igunga, Benjamini Madama, amesema kuwa mashine hizo zina uwezo wa kupima kiwango halisi cha unyevunyevu kilichopo kwenye pamba na kubaini kama mkulima ameongeza maji kwa makusudi ili kuongeza uzito wa pamba anayopeleka kuuza.

“Pamba inapovunwa shambani huwa na wastani wa unyevunyevu wa kiwango cha 8, endapo mkulima ameichanganya na maji, kipimo hiki huonyesha zaidi ya kiwango hicho, na tunaanza kuwa na wasiwasi wa uchafuzi wa pamba,” amesema Madama.

Ameongeza kuwa hatua kali huchukuliwa kwa mkulima au chama cha msingi (Amcos) kitakachohusika, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini au kufikishwa mahakamani

Aidha, amesema kuwa kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), Maafisa Ugani wameongezeka na kusaidia usimamizi thabiti wa ukusanyaji na uuzaji wa pamba kupitia vyama vya msingi

Maafisa hao pia wamepewa jukumu la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu usafi wa pamba na namna bora ya kuvuna ili kuepuka kuchanganya na vikonyo au mchanga.

Katibu Meneja wa Chama cha Msingi Iguna Balimi, wilayani Igunga, Bi. Adelia Nestory, ameipongeza serikali kwa kuleta mashine hizo, akisema zimekuwa msaada mkubwa katika kubaini udanganyifu wa kuchanganya maji kwenye pamba

Kwa upande wao, wakulima wa vijiji vya Mwajoja wilayani humo wameeleza namna elimu inayotolewa na Maafisa Ugani imechangia kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba

Gamaya Marco amesema zamani wakulima walikuwa wanachuma pamba kwa ukombakomba bila kufuata taratibu sahihi, hali iliyochangia upotevu wa ubora.

“Nimelima ekari tatu na natarajia kuvuna kilo 3000. Uchafu kwenye pamba umepungua sana, na tunaona faida ya juhudi hizi za elimu,” amesema Paulina Mathias, mkulima kutoka kijiji cha Mwajoja