Programu ijulikanayo kama IMARISHA UCHUMI NA MAMA SAMIA (IMASA) ni programu iliyoletwa kwa jitihada za Serikali ili kuwawezesha wananchi kujikomboa kiuchumi. Akitoa maelezo kwa vyombo vya Habari Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi. Beng'i Issa aamesema programu hii itahusisha mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani na kwa upande wa visiwani Baraza litashirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Zanzibar. Kwa kuanzia Baraza linafanya kazi na Ofisi ya Rais kupitia Mshauri wa Rais masuala ya wanawake na makundi maalum Mhe. Sophia Mjema. Baraza na Mshauri wa Rais wanapita kila Mkoa kuchukua taarifa za mahitaji ya Mkoa husika na kuyasajili katika mfumo maalum ulioandaliwa na serikali mtandao kwa ajili ya kuchakata taarifa hizo. Ameeleza kuwa kila Mkoa una mahitaji yake maalum kulingana na shughuli za kiuchumi zinazofanywa eneo husika. Baada ya hapo Taarifa itawasilishwa kwa Mhe. Rais na hatimaye kuona namna gani ya kuwawezesha Wananchi hao Kiuchumi. Aliongeza kuwa pamoja na jitihada ambazo zimeendelea kuchukuliwa na Serikali kuwainua wananchi Kiuchumi, bado kuna haja ya kuongeza nguvu ili kufikia malengo kama nchi hivyo programu hii ni sehemu ya jitihada hizo na itahusika na uwezeshaji wa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum. Aidha katika kutekeleza azma hiyo Taasisi za serikali na zisizo sa serikali zitashiriki kuhakikisha wananchi wanawezeshwa ipasavyo. Katibu Mtendaji aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi pindi wanapopita katika Mikoa yao ili kuhsishwa kikamilifu katika kukusanya taarifa.
Imewekwa: 10 Oct, 2024