Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuendeleza Ushirikiano na TLS
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kwa lengo la kuendelea kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kuangalia namna gani itatumia taaluma ya sheria kwa maslahi ya Taifa ili kuvutia wawekezaji wa sekta mbalimba nchini.
Hayo yamesemwa leo na Wakili Mkuu wa Serikali wakati akizungumza na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na ujumbe wake katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Dkt. Possi amesema kuwa maeneo ambayo wamepanga kushirikiana ni kukuza taaluma ya sheria kwa wanasheria ambao wamesoma na kuhitimu kwa kuendelea kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali ili waweze kutumia vyema taaluma ya sheria kulinda rasilimali za nchi kwa kusimamia vyema sekta ya sheria ili kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.
Ameeleza kuwa hivi sasa Dunia imebadilika kwa kuwa tunawawekezaji wa kimataifa wanaokuja kuwekeza Tanzania na pia wapo wawekezaji wetu ambao wanakwenda kuwekeza nje ya Tanzania hivyo kwa kuwajengea uwezo mawakili wetu kutasaidia wawekezaji hawa kuhudumiwa na watanzania ndani na nje ya nchi na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Sisi hatutaki mwekezaji anayetoka nje ya Tanzania atumie mwasheria wa kigeni, wanasheria wa Tanzania wapo, Law school ipo na inatoa wahitimu wanasheria ambao ni watanzania”. Amesema Dkt. Possi.
Akizumza kuhusu umuhimu wa kutunza maadili kwa mawakili nchini Dkt, amesema kuwa tunajukumu muhimu kutunza maadili ya mawakili waliopo na wanaokuja na kutambua umuhimu wa kazi yetu hii itatusaidia kujenga uaminifu na kukuza thamani yetu kwa wananchi tunaowahudumia.
Aidha, kiongozi huyo amewataka viongozi wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) waendelee kuishauri Serikali kuhusu namna inavyoweza kuboresha shauri mbalimbali zilizopo ili kusaidia kuendana na wakati tuliopo kwa lengo la kusaidia kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi wote.
Dkt. Possi ametumia mkutano huo kukipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) na TLS kwa kuingia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali huku akiahidi ksimamia mashirikiano hayo ili kuhakikisha wanaimarisha sekta ya sheria nchini.
Naye, Rais wa TLS nchini Bw. Boniphace Mwabukusi akizungumza katika kikao hicho ameiomba serikali kuendelea kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao huku akiweka wazi kuwa tayari wamemubaliana na Chama cha Mwakili wa Serikali kushirikiana katika masuala mbalimbali ambayo yatasaidia kuendeleza sekta ya sheria nchini.