Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

WADAU TOENI MAONI YA KANUNI ZA UREJESHAJI GHARAMA ZA UENDESHAJI MASHAURI YA SERIKALI

Imewekwa: 02 November, 2024
WADAU TOENI MAONI YA KANUNI ZA UREJESHAJI GHARAMA ZA UENDESHAJI MASHAURI YA SERIKALI

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amefungua kikao kazi cha wadau wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) cha kupitia na kutoa maoni kuhusu Kanuni za Urejeshaji wa Gharama za Uendeshaji Mashauri ya Serikali kilichofanyika mkoa wa Pwani.

 Dkt. Possi amesema kuwa ibara ya 64 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imelipa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka ya kutunga sheria mbali mbali ambapo kutokana na upekee wa uendeshaji wa Serikali na kwa mujibu wa ibara ya 97 (5) jukumu hilo limekasimiwa kwa mamlaka nyingine ambapo Bunge imetunga Sheria ya Kusimamia Mwenendo wa Mashauri ya Serikali na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.

Pia, Bunge imetunga Sheria ya Malipo ya Mawakili ya Mwaka 2015 ambapo Sheria hii kwa kiwango kikubwa imezingatia mahusiano kati ya Mawakili wa kujitegemea na mteja wake ambapo gharama hizo hulipwa kwao na sheria zilizopo hazijaweka wazi mahusiano ya kisheria kati ya OWMS na wateja inaowawakilisha mahakamani na namna Serikali itakavyorejeshewa gharama za uendeshaji wa mashauri hayo.

“Serikali inaingia gharama za kuendesha mashauri yake yaliyopo kwenye mabaraza ya usuluhishi na mahakama mbali mbali nchini hivyo OWMS imeona umuhimu wa kuandaa kikao hiki cha wadau ili mtoe maoni ya kuboresha Kanuni za Urejeshaji Gharama za Uendeshaji Mashauri ya Serikali ili taasisi za Serikali na wadau wanaohusika na uendeshaji wa mashauri waweze kulipa gharama za uendeshaji wa mashauri kwa kuwa Serikali inatumia fedha kuendesha mashauri hayo ambayo yanachukua zaidi ya miaka miwili kuendeshwa, tunawashukuru kwa kuitikia wito na kushiriki kikao hiki”, amefafanua Dkt. Possi.

Pia, ametoa rai kwa wadau hao kujadili kwa kina na kutoa maoni kuhusu kanuni hizo ili wakati wa utekelezaji wake ziweze kuwa wazi na rahisi kutekelezwa. Wadau walioshiriki kikao hicho wanatoka taasisi mbali mbali za Serikali zinazohusika na mnyororo wa utoaji haki na kitafanyika kwa siku mbili.