Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Wananchi watakiwa kuendelea na zoezi la kupata elimu ya mpiga kura ili washiriki Uchaguzi wa Serikali za Mtaa.

Imewekwa: 25 October, 2024
Wananchi watakiwa kuendelea na zoezi la kupata elimu ya mpiga kura ili washiriki Uchaguzi wa Serikali za Mtaa.

Wananchi wametakiwa kuendelea kupata elimu kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu licha la Mahakama kuruhusu waleta maombi katika shauri linalopinga mamlaka ya Waziri wa TAMISEMI kutunga kanuni za kuratibu, kusimamia nakuendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini kuruhusiwa kufungua shauri la msingi kwa kuwa mchakato mzima wa uchaguzi haujasimamishwa.

Hayo yamesemwa na Wakili wa Serikali Mkuu Bw. Deodatus Nyoni mara baada ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa shauri la awali lililofunguliwa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam na wananchi watatu wakiongozwa na Bob Chacha Wangwe wakipinga Mamlaka ya Waziri wa TAMISEMI kusimamia na kuendesha uchaguzi tajwa hapo juu.

Wakili Wa Serikali Mkuu Bw. Deodatus Nyoni ameeleza kuwa ni muhimu wananchi hao wakaendelea na mchakato mzima wa kupata elimu ya mpiga kura na kufuata taratibu nyingine kwa kuwa katika uamuzi uliotolewa leo Septemba 09,2024 na Mhe Jaji Wilfredy Dyasobera mchato mzima wa uchaguzi huu haujasimamishwa.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa shauri la awali Wakili huyo ameendelea kuwahimiza wananchi kote nchini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha mara zoezi hilo litakapofunguliwa ili waweze kutumia haki yao ya msingi kikatiba kuchagua viongozi sahihi watakaosaidia kuwaletea maendeleo.

Ameleza kuwa licha ya Mahakama kukubaliana na hoja za waleta maombi ambazo amezitaja kuwa ni pamoja na wahusika kuleta maombi yao ndani ya muda pamoja na kuwa na hoja za msingi lakini wao kama upande wa Serikali bado wanaamini mapingamizi yao yalikuwa na msingi na hivyo wao wanaheshimu maamuzi ya Mahakama hiyo kama yalivyotolewa na Mhe.Dyasobera.

Ameongeza kuwa pamoja na hoja zao kukubaliwa bado Mahakama imetupilia mbali aya nne  zilizokuwa katika shauri hilo ambazo ni aya ya 10,15,17 na 19 kwa kuwa zilikuwa na shida na hivyo hazitakuwa sehemu ya nyaraka zitakazowasilishwa katika shauri la msingi kama waleta maombi wakiamua kufungua shauri husika.

Ameendelea kueleza kuwa maombi haya ya kusimamisha uchaguzi kwa jinsi walivyokuwa wanayaomba hayakuwa sehemu ya maombi yao ya msingi hivyo ameendelea kuitaka serikali kuendelea na taratibu zote inazoendelea kufanya ikiwa ni pamoja na kuendelea kuratibu zoezi la kuhamasisha wananchi ili ikifika muda mwafaka wananchi waweze kushiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadae mwakani washiriki zoezri la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Amehitimisha kwa kusema kuwa kwa kuwa upande wa waleta maombi wameelekezwa kuleta maombi yao mapema wao kama Mawakili wa Serikali wako tayari kuyafanyia kazi kama vile yatavyokuwa yamekuja ili kuhakikisha haki inapatikana na uchaguzi uweze kufanyika kama ulivyopangwa katika kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.