UZINDUZI WA BARAZA
Baraza la Wafanyakazi la Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma ma Sekta Binafsi (PPP Centre) limezinduliwa rasmi Aprili 25, 2025 Jijini Dodoma, huku wajumbe wa Baraza hilo wakiaswa kuwa kioo katika kuhakikisha miradi ya ubia inatekelezwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugnezi Mtendaji wa PPPC, Bw. David Kafulila, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (DCS) Bi. Shoma Kibende, amewataka wajumbe wa Baraza hilo kujadili hoja za msingi kwa umakini na weledi ili kuhakikisha majukumu ya Taasisi hiyo yanatekelezwa ipasavyo kwa ushirikiano ili kuleta utendaji kazi ulio bora baina ya wafanyakazi.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Taasisi aliongeza kuwa, Baraza la Wafanyakazi ndio chomo pekee kwa mujibu wa Sheria ambalo linawajibu wa kuwasilisha hoja za kuboresha Taasisi, Mazingira ya Kazi pamoja na ustawi wa Wafanyakazi na kumaliza chamgamoto ndogo ndgo ambazo zinaweza kujitokeza ndani ya Taasisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa, Bw. Joel Kaminyoge amewataka wajumbe wa Baraza hili kuwa kielelezo muhimu katika kushauri ili jukumu kubwa la Taasisi katika kuratibu, kuhamasisha na kusimamia miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi linafikiwa.
Bw. Kaminyoge aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa PPPC Watanzania wengi wana matumaini makubwa kwa Taasisi hivyo Baraza hilo kwa kushirikiana na Menejimenti lina wajibu wa kuhakikisha kuwa miradi ya ubia inatekelezwa kwa uwazi, ufanisi na kwa manufaa ya jamii nzima.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa kikao walipata mafunzo maalum juu ya mapambano dhidi ya rushwa yaliyotolewa na Bi. Idda Michael Siriwa kutoka TAKUKURU, ambapo alisisitiza kuwa jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mmoja na kwamba kila mfanyakazi anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha maadili na uwajibikaji vinazingatiwa katika kila hatua ya utekelezaji wa majukumu.
Baraza hilo lililofanyika kwa siku mbili limeweza kujadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti inayoendelea kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikieleza mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kipindi hicho.
Aidha, kupitia Baraza hilo limeweza kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2025/2026, kwa lengo la kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Taasisi inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
