Sababu za upimaji wa Mionzi kwenye bidhaa
Published on November 26, 2019

Serikali imewataka wafanyabiashara wa zao la Tumbuka nchini pamoja na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kukutana kwa pamoja kwa lengo la kuboresha biashara ya bidhaa ya tumbaku na kueleza kuwa ugomvi kati ya TAEC na wafanyabiashara wa zao la Tumbaku sasa haupo tena kwani sasa watakaa pamoja kwa lengo la kufanya mikutano ya kuboresha taratibu zao.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (Mb) ametoa agizo hilo katika mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa zao la tumbaku ambapo TAEC iliwasilisha mada juu ya majukumu inayotekeleza kisheria na sababu za tozo kwenye bidhaa ya Tumbaku kwa wafanyabisahara ambapo amesema lazima TAEC na wafanyabiashara kuweka mikakati ya pamoja kwa lengo la kuboresha.
Waziri Bashe alipata nafasi ya kusikiliza maoni mbali mbali ya wafanyabiashara wa zao hilo na kuona namna gani wataweza kuwa na ushirikiano mzuri kwa lengo la kupekeka maendeleo mbele katika utoaji huduma baina ya TAEC na wafanya biashara wa zao la Tumbaku hapa nchini.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala aliwaeleza wadau katika mkutano huo sababu mbalimbali za kiusalama juu ya udhibiti wa vyanzo vya mionzi nchini na upimaji wa mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa za chakula na sababu za kuwatoza asilimia 0.2
Hata hivyo pia Prof. Busagala amewaeleza wadau hao wa zao la Tumbaku mambo kadhaa ambayo husababisha uchafuzi wa mionzi katika bidhaa hizo, na sababu za udhibiti wa bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na kulinda watumiaji wa bidhaa hizo dhidi ya athari inayoweza kusababishwa na mionzi. Sheria namba 7 ya Nguvu za Atomiki ya 2003 inaipa mamlaka TAEC kupima mionzi katika bidhaa za mnyororo wa chakula, na pia kulinda bidhaa hiyo katika soko la kimataifa dhidi ya mionzi.
Mkutano huo wa mwaka uliwakutanisha washiriki 150 kutoka katika tasnia ya tumbaku, wakiwemo wakulima wa tumbaku, wafanyabiashara wa tumbaku, Bodi ya Tumbaku, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Halmashauri za Wilaya na Manispaa, Baraza la Ushindani , Viongozi wa Ushirika, Vyuo Vikuu, Wizara ya Kilimo, Taasisi ya Utafiti na Wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mhe. Bashe Alihitimisha kwa kusema kwamba, ugomvi ambao alikuwa nayo na watu wa mionzi sasa umekwisha