Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / TAEC kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yafungua Rasmi Dirisha la Maombi ya Nafasi za Ufadhili wa Samia Extended

TAEC kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yafungua Rasmi Dirisha la Maombi ya Nafasi za Ufadhili wa Samia Extended

TAEC kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yafungua Rasmi Dirisha la Maombi ya Nafasi za Ufadhili wa Samia Extended

Published on July 29, 2024

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua rasmi dirisha kwa waombaji wenye sifa za kuomba nafasi za kusomea Shahada ya Juu ya Teknolojia ya Sayansi ya Nyuklia kupitia ufadhili wa Samia Scholarship Extended (SSE) 2024/25.

Katika mwaka fedha 2024/25, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi bilioni 1.6 ili kuiwezesha TAEC kufadhili wanafunzi watano kwenda nje ya nchi kusoma Shahada ya Uzamili katika fani mbalimbali zinazohusiana na teknolojia ya Nyuklia.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. ametangaza rasmi juu ya kufunguliwa kwa dirisha la kuomba nafasi hizo muhimu na kusema ufadhili huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa sekta ya sayansi ya mionzi hapa nchini.

"Tangu mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilianza programu ya kutoa ufadhili kwa asilimia 100 kwa wanafunzi bora katika masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya kidato Cha sita,” alisema.

Ufadhili huo unawalenga wanafunzi wenye sifa ambao wamechagua kufanya shahada ya kwanza katika masomo ya Sayansi, Habari na Teknolojia (IT), Uhandisi na Hisabati, pamoja na Elimu Tiba.

Mpaka sasa Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalam katika sekta ya sayansi ya nyuklia, hivyo kulazimu serikali kuja na mpango madhubuti wa kusaidia kupunguza hitaji hilo,

Kwa sasa Tanzania ina wataalam sita tu wa Medical Physics pamoja na Nuclear Medical Doctors ambapo  mtaalamu mmoja ni wa Radiochemistry, na Madaktari wawili tu wa Radiopharmacists.

"Uhitaji wa teknolojia ya sayansi ya nyuklia nchini Tanzania unaendelea kuongezeka kwa kasi kila siku kwa hivyo, lazima tutengeneze idadi kubwa ya wataalam wa hali ya juu," Prof Mkenda alisisitiza.

Akitoa maelezo juu ya utaratibu uliowekwa wa kuomba nafasi za ufadhili huo,  Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof Najat Kassim Mohammed, ameeleza kuwa waombaji wenye sifa wanapaswa kujaza fomu husika zinazopatikana kupitia tovuti ya TAEC na pia wanaweza kupata fomu hizo kupitia tovuti ya Wizara ya Elimu.

"Ufadhili huu utawanufaisha wanafunzi (wataalamu) wanaotaka kusoma maeneo angalau matano yanayohusu sayansi na teknolojia ya nyukilia na waombaji wanatakiwa kuomba kusoma katika Vyuo vinavyosimamia udhamini huo ni vile vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), katika nchi kadhaa, zikiwemo Australia, Canada, China, Ufaransa, India, Finland na Korea Kusini. miongoni mwa wengine” amesema Prof. Najat.