Mwanzo / Huduma Zetu / 56 WACHUNGUZWA MACHO 15 WAKIFANYIWA UPASUAJI MTOTO WA JICHO NEWALA

56 WACHUNGUZWA MACHO 15 WAKIFANYIWA UPASUAJI MTOTO WA JICHO NEWALA

56 WACHUNGUZWA MACHO 15 WAKIFANYIWA UPASUAJI MTOTO WA JICHO NEWALA

Published on June 05, 2023

Article cover image

Mtwara, 30 Mei, 2023

Madaktari Bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa (BMH) leo Mei 30, 2023 wameanza kambi maalum ya kutoa Huduma ya Upasuaji wa macho kwa wagonjwa wanaohitaji Huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Newala Mtwara.

Kambii hii itadumu kwa muda wa siku tano ambapo imeanza leo Mei 30, 2023 na itamalizika Juni 2, 2023.

Dkt. Amon Mwakakonyole ambae ni daktari bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka BMH ameeleza kuwa kambi hii ni muendelezo wa kambi iliyofanyika Mei 15 – 19 2023. 

“Hapo awali tulifanya kambi hapa Hospitali ya wilaya ya Newala na tulifanya uchunguzi kwa wagonjwa 386 na kati yao wagonjwa 35 walipatikana na tatizo la mtoto wa jicho hivyo walihitaji upasuaji ili kurejesha vizuri uoni wao” aliongeza Dkt. Mwakakonyole.

Mpaka sasa wagonjwa 15 wamejitokeza kwaajili ya upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho na mpaka muda huu upasuaji unaendelea theater aliendelea Dkt. Mwakakonyole.

“Licha ya kambi hii kuwa mahususi kwaajili ya upasuaji tutafanya pia uchunguzi kwa wagonjwa mbalimbali na kuwapatia huduma stahiki na kwa wenye tatizo linalohitaji upasuaji atapatiwa huduma hiyo,” alisema Dkt. Mwakakonyole.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Newala Dkt. Ramadhan Shaban amewaalika wataalamu kutoka BMH na kutambua mchango wao katika kambi iliyopita.

“Kutokana na kazi kubwa iliyofanyika kwenye kambi iliyopita ndio maana leo hii tupo hapa hivyo niwakaribishe sana na niwahakikishie usalama wenu,” alisema Dkt. Shaban.

“Nimepokea simu za watu mbalimbali wengine kutoka masasi wakinihakikishia kua watakuja kupata matibabu katika kipindi hiki cha kambi,” aliongeza Dkt. Shaban.

Baadhi ya wagonjwa wameshukuru kuwepo kwa kambi hii kwani kumewasaidia kutambua magonjwa yanayowasumbua na kupatiwa matibabu.

“Nashukuru uwepo wa kambi hii na madaktari kutoka BMH kwani nimepatiwa matibabu vizuri na natarajia matibabu haya yatanisaidia na kuondokana na tatizo hili,” alisema Amina Mohamed mmoja wa wagonjwa waliojitokeza kupata Huduma.

Mpaka sasa wagonjwa 56 wamefanyiwa uchunguzi kwa siku ya leo.