HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YAPOKEA MSAADA WA MASHINE YA KISASA YA KIDIGITALI (DIGITAL SCANNER) KWA AJILI YA UCHUNGUZI WA PATHOLOJIA KUTOKA TAASISI YA WAPATHOLOJIA BILA MIPAKA YA NCHINI ITALIA.
Published on March 04, 2025

Habari na Ludovick Kazoka, Dodoma, 13/02/2025
Maabara ya Patholojia ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imepokea msaada wa Mashine ya Kisasa ya Kidigitali ya kufanyia vipimo kitaalamu ikijulikana kama Digital Pathology Scanner kutoka kwa Chama cha Wapatholojia Wasio na Mipaka (Association of Pathologists Beyond Borders) cha nchini Italia.
Akiongea baada ya kupokea kifaa tiba hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt Kessy Shija, amesema kuwa mashine hiyo itaongeza ubora na ufanisi wa vipimo vya Patholojia, itarahisisha kushauriana baina ya watalaam wa BMH na hata nje ya BMH kupitia mitandao (electronic consultation) katika kubainisha ugonjwa, itasaidia kupata uzoefu kwa watalaam wa BMH kutoka kwa watalaam wazoefu duniani kote kwa kufanya mashauriani kwa njia ya mtandao.
Dkt. Shija ameongeza kuwa mashine hiyo itasaidia katika kufundishia teknolojia mpya za vipimo kwa Wataalamu wa Afya walio mafunzoni na hata kutumika katika kufanyia Tafiti mbalimbali za kisayansi katika sekta ya Afya.
"Kifaa tiba hicho pia kitapunguza gharama na muda wa wagonjwa kusubiria majibu kama ilivyokuwa zamani kwa kuwezesha picha za sampuli na majibu kuweza kusafirishwa kidigitali badala ya kuisafirisha sampuli yenyewe kuipeleka kwenye uchunguzi zaidi maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi" amesema Dkt. Shija kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi.
Dkt. Shija ametumia fursa hiyo kuwashukuru Chama cha Wapathologia wasio na Mipaka kwa kutoa mashine hiyo kwa BMH.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Pathologia wasio na Mipaka, Dkt Paolo Giovenali, akikabidhi mashine hiyo amesema kuwa, kupitia mashine hiyo, Madaktari wa Pathologia wa BMH wanaweza kushirikisha wataalamu wenzao kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nchi mbalimbali Duniani kwa kuwa wataweza kuwasiliana Kidigitali kwa kutumia picha zilizopigwa na mashine hiyo.
"Mashine hii pia ina programu ya "Akili Mnemba" (Artificial Intelligence - AI) hivyo kumuongezea wigo zaidi mtaalamu wa Patholojia katika vipimo anavyofanya," amesema Dkt. Giovenali huku akisisitiza teknolojia za aina hiyo zinasaidia kutengeneza Network za Wataalamu Duniani kote.
Dkt Henry Joseph, Daktari Bingwa wa Pathologia wa BMH, amesema kuwa mashine hiyo imewaongezea wigo kwa kuwa wataalamu wa BMH wataweza kushirikisha wenzao kokote Duniani kupitia picha zitakazo pigwa na mashine hiyo.