BMH KUZALISHA WATAALAMU WA RADIOGRAFIA
Published on November 03, 2022
Dodoma - BMH Novemba 3, 2022
Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma imezindua Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi kitakachozalisha wataalamu wa Radiografia pamoja na kada zilizo na wataalamu wachache ili kuondoa changamoto ya rasilimaliwatu kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya nchini.
Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa Chuo hicho, Profesa Paschal Luggajo, Mkurgunzi wa Tiba Wizara ya Afya amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeziwezesha Hospitali zote kuanzia za Mikoa hadi Taifa kuwa na MRI, CT-SCAN na X-RAY ambapo hali hii inapelekea kuwa na uhitaji mkubwa wa wataalamu wa vifaa hivyo.
“Niwakumbushe takwimu za sensa zilizotoka tarehe 31 Oktoba, 2022 zinaonesha kuwa nchi ina Zahanati 7,889, Vituo vya Afya 1,490 na Hospitali 688 na vituo vyote hivi vinahitaji wataalamu wenye ujuzi wa kutumia vifaa hivyo” Alisema Profesa Luggajo.
Aidha, Profesa Luggajo ameutaka uongozi wa Chuo hicho kuhakikisha unaepuka kudahili wanafunzi wengi kwa lengo la kupata fedha bila kujali ubora wa mafunzo utakaopelekea upatikanaji wa wataalamu wenye umahiri na weledi wa kutosha, akiwataka wanafunzi kutumia miundombinu iliyopo Hospitalini kwa kuwa ni ya kisasa inayowapa fursa na mazingira bora ya kujifunza.
“Nimezunguka nimeridhishwa na mazingira ya kujifunzia, hayawezi kuwa bora zaidi ya yaliyopo hapa, nahimiza nidhamu kwa wanafunzi, kazi zetu za huduma za Afya zimezungukwa na maadili, kuna siri za wagonjwa na viapo” Alisema Profesa Luggajo.
Awali akitoa taarifa kuhusu Chuo hicho cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Benjamin Mkapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika, alisema changamoto ya upatikanaji wa wataalamu wa kada za ngazi ya Cheti na Diploma kujaza nafasi za ajira katika Hospitali yake ilionesha uhaba mkubwa wa Radiographers na Anaeathetist na hivyo kulazimika kuomba vibali vya kuhamishia wataalamu kutoka vituo vingine ambavyo navyo vilikuwa na uhaba.
“Tuliona ni jukumu letu kama Hospitali ya Rufaa kuanzisha mafunzo haya ili kuongeza wataalamu hasa baada ya kuboreshwa miundombinu ya kutolea huduma za Afya nchini” Alisema Dkt. Chandika.
Kuanzisha mafunzo ya Stashahada ya Radiolojia na Uchunguzi wa Magonjwa (Diploma in Diagnostic Radiography) na kwa kuwa hakukuwa na mtaala wa kutoa mafunzo hayo kwa ngazi ya Diploma kwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTEVET), Hospitali ya Benjamin Mkapa ililazimika kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo - Wizara ya Afya, NACTEVET na wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu kutoka Bugando CUHAS, MNH (MUCOHAS), KCMC Hospitali ili kutengeneza mtaala huo.
Mtaala huo umepewa ithibati na Balaza la Taifa la Elimu na Ufundi (NACTEVET) kwa namba ya rejea HASP 33.7/14445 tarehe 31 Januari, 2022 na utatumika kwa miaka 5 hadi tarehe 31 Januari 2027.