BMH YASIFIWA KWA KUTUNZA MAZINGIRA
Published on August 12, 2022
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), Bi Marry Maganga, ameisifia Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kutunza mazingira vizuri hivyo kufanya eneo linalozunguka hospitalini hapo kuwa salama.
Bi Maganga ametoa sifa hizo wakati alipotembelea hospitalini hapo mwisho wa mwezi Mei wakati wa Wiki ya Mazingira, akisema Serikali itaitumia Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati kama rejea ya Utunzanzaji Mazingira.
“Tunajivunia kuwa na taasisi (BMH) inayotunza mazingira vizuri, yenye mfumo mzuri wa kutibu majitaka…Nawapongeza BMH,” alisema Katibu Mkuu baada ya kutembelea Hospitali hiyo ya Umma na kupanda mti katika eneo la Hospitali.
Bi Maganga ameagiza uongozo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kulinda eneo la BMH la kutibu majitaka ili watu watu wenye tabia ya kuvamia maeneo wasiweze kulivamia eneo hilo kwa sababu mji unakua kwa kasi.
“Hii inatuonyesha kuwa tupo salama tunapopata huduma za afya hapa Hospitali ya Benjamin Mkapa.Kutoka jikoni mpaka kantini, mazingira ni safi,” alisema Katibu Mkuu.
Bi Maganga pia aliipongeza BMH kwa kutumia nishati jadidifu katika majiko ya Hospitali na kwamba BMH inatunza mazingira kwa kutokutumia kuni, ambazo zinasababisha mmomonyoko wa udungo and uchafuzi wa mazingira zinapochomwa.
“Tutaitumia BMH kama taasisi ya mfano tunaposhawishi taasisi nyingine kutunza mazingira,” aliongeza Katibu Mkuu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dkt Kessy Shija, alitoa shukrani kwa Katibu Mkuu kwa kuchagua kuitembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa na kwamba watakeleza maagizo yake.
“Tutakeleza kwa vitendo maagizo yote ambayo umetupa na tutaendeleza kutunza mazingira eneo la Hospitali,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH.
BMH imebakia kuwa ndiyo hospitali pekee nchini inayopandikiza figo kwa kutumia wataalamu wake wazawa. Ilianza huduma hii kwa usaidizi wa Shirika la afya la Japan la Tokushukai mwaka 2019. Ilikuwa ni hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma hii baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.