Mwanzo / Huduma Zetu / BMH YAPANDIKIZA UUME KWA MARA YA KWANZA NCHINI

BMH YAPANDIKIZA UUME KWA MARA YA KWANZA NCHINI

BMH YAPANDIKIZA UUME KWA MARA YA KWANZA NCHINI

Published on June 15, 2023

Article cover image

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)kwa kushirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo nchini (TAUS) pamoja na dkt. Bingwa kutoka Ufaransa kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza uume kwa watu wawili ambao uume ulishindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.

Akizungumza baada ya kukamilisha upasuaji Dkt. Remidius Rugakingira daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.

“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyo wezesha uume kurudi katika hali yake upasuaji huu tumeshirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo pamoja na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo kutoka Ufaransa na tumefanikiwa katika hilo,” alieleza Dkt. Rugakingira

Dkt. Rugakingira aliendelea kwa kusema kuwa huu ni wito kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania.

Kwa upande wake Dkt. Liuba Nyamsogolo ambae ni kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) amesema kuwa wamefikia hatua hii kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.

“Moja wapo ya dhumuni ya TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana ma wataalam kutoka nje ili kuleta teknolojia inayopatikana duniani nchini Tanzania na kutibu magonjwa kama haya kwa wale wenye matatizo,” alisema Dkt. Nyamsogolo.

Msemaji wa BMH Bw. Jeremiah Mbwambo ameeleza "Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume, serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha teknolojia za kisasa za matibabu ili kuwapatia matibabu thabiti wananchi"