DKT CHANDIKA AAGWA NA BODI YA WADHAMINI BMH
Published on June 14, 2024
Mkurugenzi Mtendaji aliyemaliza muda wake Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika, ameagwa rasmi leo na Bodi ya Wadhamini ya Hospitali.
Akiongea na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano BMH, Dkt. Alphonce Chandika ametoa rai kwa watumishi kutoa ushirikiano kwa Mkurugenzi mpya Prof Makubi.
"Namshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniruhusu ni huduma katika kipindi cha mwisho cha kuiongoza BMH. Aidha, niwasisitize watumishi wa BMH kumpa ushirikiano Prof Makubi ili adhima yake ya kuiongoza BMH katika kipindi chake ifikiwe kwa haraka" alisema Dkt. Chandika.
Dkt Chandika, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda ya Kati, amehudumu kwa miaka 8. Ameagwa leo BMH. Katika kikao hicho alimpogeza Dr Chandika kwa kukamilisha majukumu yake vyema na kumuombea kheri katika utumishi mwingine atakavyopangiwa.
Wakati huo huo, Bodi ya Udhamini ya Hospitali, imetembelea mradi wa ujenzi wa kitakachokuwa Kituo cha Matibabu ya Saratani cha BMH na vyumba vinavyojengwa vya upasuaji.
Mkurugenzi Mtendaji, Prof Makubi, amemuagiza Mkandarasi, Mohamed Builders, anayejenga jengo la Kituo cha Saratani cha BMH, kuwasilisha madai yake siku ya alhamisi ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliopangwa.
Jengo hilo la ghorofa 3 linatarajiwa kukamilika mwakani, mwezi wa 6. Litakapokamilika mbali na kuwa Kituo cha Saratani, pia litaongeza idadi ya wodi hivyo kufikisha vitanda 550 kutoka 400 vya sasa.