Mwanzo / Huduma Zetu / WAGONJWA 572 WANUFAIKA MATIBABU YA MACHO KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA WA BMH

WAGONJWA 572 WANUFAIKA MATIBABU YA MACHO KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA WA BMH

WAGONJWA 572 WANUFAIKA MATIBABU YA MACHO KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA WA BMH

Published on June 05, 2023

Article cover image

Kambi ya madaktari Bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) iliyofanyika wilaya ya Newala, Mtwara leo Juni 2, 2023 imefikia tamati na imefanikiwa kuwahudumia wagonjwa 572 ndani ya kipindi cha siku nne.

Kambi hiyo iliyoanza Mei 30, 2023 imeonesha mafanikio makubwa  kwani wananchi wa Newala wamepatiwa matibabu kwa gharama nafuu lakini pia wahudumu wa afya kujengewa uwezo katika kutoa Huduma.

Dkt. Amon Mwakakonyole ambae ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho amesema kuwa katika kambi hii ya siku nne magonjwa yaliyokua yanaongoza ni uoni hafifu unaorekebishwa kwa miwani, mtoto wa jicho, presha ya macho na aleji.

“Tumeona wagonjwa wenye uoni hafifu na tumewapatia miwani, kwa wale wenye mtoto wa jiicho tumewafanyia upasuaji ili kuondoa mtoto wa jicho na kuwawekea lens na wenye aleji tumewapatia dawa,” alieleza Dkt. Mwakakonyole 

Katika kambi hii tumefanya upasuaji kwa wagonjwa 33 na upasuaji umeonekana kuwa wa mafanikio kwa wagonjwa wengi na tumetoa miwani 61 kwa wagonjwa walioonekana kuhitaji.

“Tumefanya upasuaji kwa wagonjwa 27 ambao walikua na mtoto wa jicho na 6 tuliwatoa kinyama kwenye jicho,” aliongeza Dkt. Mwakakonyole

Dkt Mwakakonyole alisisistiza kuwa kutakua na ongezeko la wagonjwa katika Kliniki ya macho katika Hospitali ya Wilaya ya Newala kutokana na wale waliofanyiwa upasuaji na wale watakaohitaji matibabu ya kila mwezi.

Leo hii tunatamatisha kambi yetu katika Wilaya hii ya Newala hivyo tunashukuru wananchi wa Newala kwa kutuamini na kujitokeza kupata matibabu kutoka kwetu kwani imekua faraja kubwa sana.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Newala Dkt Ramadhan Shabani amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa BMH na menejimenti nzima kwa kuruhusu madaktari wa BMH kufanya kambi Newala.

“Namshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa BMH kwa kuwa na mawazo chanya juu ya kambi hii kwakua tumefaidika sana kwani watoa huduma wetu wamejengewa uwezo mkubwa na wananchi wetu takribani 500 wenye uwezo wa chini wamesogezewa huduma karibu yao,” alieleza Dkt. Ramadhan

Tunapanga kuendeleza mashirikiano hayo kwenye maeneo mengine kama upande wa magonjwa ya meno, ngozi, pamoja na magonjwa ya masikio, pua na koo aliongeza Dkt. Ramadhan

Baadhi ya wananchi wameshukuru uwepo wa Madaktari Bingwa kwani wamenufaika haswa wale wenye hali ngumu kiuchumi.

“Nilikua na tatizo la macho tangu mwaka 2008, nilikua sioni mbali na macho yalikua yamejaa ukungu. Kabla ya kufanyiwa upasuaji nilikua sioni mawe na nilikua naruka shimo sehemu ambayo haina shimo lakini baada ya upasuaji huu naona kila mtu vizuri na ninayaona mawe vizuri wakati wa kutembea. Nashukuru madaktari kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa kwani sasa naweza kuona vizuri,” Asha Ismail mkazi wa Newala.

Mpaka sasa Madaktari Bingwa wa BMH wameona wagonjwa 572 tokea wameanza kambi katika Wilaya ya Newala.