Mwanzo / Huduma Zetu / WAZIRI MKUU AZINDUA HUDUMA ZA KUPANDIKIZA ULOTO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

WAZIRI MKUU AZINDUA HUDUMA ZA KUPANDIKIZA ULOTO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

WAZIRI MKUU AZINDUA HUDUMA ZA KUPANDIKIZA ULOTO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Published on May 12, 2023

Article cover image

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), 10 Mei, 2023 alizindua rasmi huduma za Upandikizaji wa Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu (Sickle cell anemia), katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika Hospitalini hapo Majira ya mchana na kupokea maelezo mafupi ya kitaalamu kuhusu huduma za upandikizaji wa Uloto kutoka kwa Wenyeji wake Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), na Waziri wa Afya, na Dkt. Alphonce Chandika Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya hiyo, baadaye alikata utepe kufungua rasmi huduma hizo.

Kisha akawaona watoto waliyopokea huduma hiyo ya kupandikizwa Uloto na waliyowachangia, Mhe. Waziri Mkuu aliwapongeza na kuwapa pole huku akiendelea kupokea maelezo ya kina kutoka kwa Madaktari waliyobobea katika matibabu ya Damu  na Upandikizaji wa Uloto.

Baadaye Mhe. Majaliwa alielekea eneo liloandaliwa na kuzungumza na Madaktari, Wataalamu wengine wa Hospitali hiyo, viongozi mbalimbali waliyofika kushuhudia uzinduzi wa rasmi wa hudumaza upandikizaji Uloto, pamoja na wananchi wa Mtaa wa Ng’ong’ona na Mapinduzi.

Katika hotuba yake kwa mashuhuda wa tukio la Uzinduzi wa huduma za Uloto Mhe. Waziri Mkuu alieza kufurahishwa kwake na ubunifu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wa kuanzisha huduma ya kibingwa ya Upandikazi wa Uloto kwani kufanya hivyo ni kuishi katika malengo ya kuanzishwa kwake.

“Hapa tunaona mafanikio makubwa, tunaona utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassa ya kuhakikisha tunasogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili wanapopatwa na matatizo wasisafiri ubali mrefu kutafuta ufumbuzi” Alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Akifafanua kauli yake hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa, kwa lugha nyingine, kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali kuwawezesha wananchi wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi, akitolea mfano wa namna huduma ya upandikizaji Uloto nchini inavyopunguza gharama kufikia shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja.

Mhe. Waziri Mkuu alihitimisha Hotuba yake kwa kutoa maelekezo mbalimbali kwa mamlaka zinazosimamia Afya nchini ikiwemo, kuhakikisha zinaendelea kutoa elimu juu ya namna ya kukinga, ikiwa ni pamoja na kuwapa nasaha vijana kupima Selimundu kabla ya kufunga ndoa, na kuhakikisha kuwa watoto wachanga wanapimwa ili kuwapa nafasi wazazi nafasi ya kufahamu mapema na kuchukua hatua stahiki.

Awali Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), ambeye ni Waziri wa Afya ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuendelea kutimiza maombi yanayopelekwa na Wizara anayoiongoza akitolea mfano wa utekelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Kituo cha Umahili wa Tiba Mionzi na tekinolojia ya Nyukilia unaondelea katika Hospitali ya Benjamin Mkapa akirejelea adhima ya kuipa hadhi ya kitaifa Hospitali hiyo.

“Tutajenga kituo cha Umahili cha Tiba za Moyo, na tunaendelea na majadiliano ya kuona uwezekano wa kujenga Hospitali nyingine ya Kisasa maalumu kwa huduma za Mama na Mtoto ndani ya Hospitali ya Benjamin Mkapa” Alifafanua Mhe. Ummy.

Katika hatua nyingine Mhe. Waziri wa Afya alitoa wito kwa wazazi wenye watoto wanosumbuliwa na Ugonjwa wa Selimundu kujitokeza na watoto wao ili kutafuta mchangiaji miongoni mwa watoto wao atakayewezesha kuokoa maisha ya mtoto mwenye ugonjwa kwa kuwa Wizara inaangalia uwezekano wa kugharamia matibabu ya Uloto kwa watoto 20 kila mwaka.

“Mtoto Ester ni shujaa wetu leo, ana umri wa miaka sita, lakini amechangia Uloto na kumsaidia mdogo wake Elisha mwenye Umri wa miaka minne, leo tunaye hapa yuko salama kama anavyooneka” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Katika taarifa yake Dkt. Aphonce B. Chandika, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa alisema kuwa Hospitali hiyo imekuwa ikipiga hatua katika kuanzisha huduma za kibingwa na bobezi katika maeneo mbali mbali kama usafishaji figo, kupandikiza figo, kuzibua mishipa ya moyo, kuziba matundu ya moyo kwa watoto na upasuaji wa mishipa ya fahamu.

“ninayo furaha kuufahamisha umma wa Tanzania na nchi jirani kuwa kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kutoa huduma ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell)”

Akafafanua kuwa aina ya upandikizaji Uloto ijulikanayo kama Allogeneic Hematopoietic Stem Cell Transplant” imefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 7 barani Afrika zinazotoa huduma hiyo ikiungana na Algeria, Afrika kusini, Misri, Moroko, Nigeria na Tunisia.