Waziri Kairuki Azindua Bodi ya DART, ataka Mikakati zaidi kuboresha Usafiri wa Umma
Waziri Kairuki Azindua Bodi ya DART, ataka Mikakati zaidi kuboresha Usafiri wa Umma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki amezindua Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), na kuiagiza iongeze bidii na ubunifu ili kuboresha huduma ya usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Novemba 15,2022 Dar es Salaam, Waziri Kairuki aliitaka Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa DART kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha usafiri wa umma Dar es Salaam unakuwa wa uhakika, nadhifu na wakuaminika wakati wote ili kuchochea maendeleo.
Alisema ni lazima Bodi isimamie kwa ukamilifu Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kwani ni mradi wa kimkakati ambao ni kioo cha Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, kwani watu wengi kutoka nchi za nje wanakuja kwa ajili ya kujifunza namna ya uendeshwaji wa mradi huo.
Aidha, Waziri Kairuki alisisitiza suala la ubunifu hasa katika matumizi ya Teknolojia mpya na za kisasa ili kuendana na adhma ya kuanzishwa kwa mradi huo iliyolenga kuwa usafiri wenye unaokidhi viwango vya kimataifa.
“Nitahakikisha nawapa kila aina ya ushirikiano mtakaohitaji katika kuusimamia Wakala wa DART ili uweze kutimiza majukumu yake ipasavyo hasa katika masuala ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato” Alisema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki alisema anauona uwezo uliopo katika ukusanyaji wa mapato hivyo ni vyema kuuimarisha ili ifike wakati Wakala wa DART uondokane kabisa na utegemezi wa fedha kutoka serikalini na badala yake uweze kutoa gawio kwa serikali.
Aidha kwa kuzingatia umuhimu wa usafiri wa umma, na uendeshaji wa biashara unaoshirikisha sekta ya umma na binafsi, ni vyema jicho la kibiashara liwepo ili kuhakikisha pande zote mbili Serikali na sekta binafsi zinanufaika kwa uwepo wa mradi huo.
Kwaupande mwingine, Waziri Kairuki pia aliutaka Wakala wa DART kupitia uzoefu ulioupata Dar es salaam, uwe chachu ya kuweza kufikiria jinsi watakavyoweza kuanzisha huduma kama hiyo katika miji mikubwa mingine inayokabiliwa na msongamano mkubwa wa magari na huduma ya usafiri wa umma isiyokuwa nadhifu.
Pia alisisitiza ukamilishwaji wa miundombinu ya mradi wa DART awamu ya pili kutoka Gerezani Kariakoo hadi Mbagala Rangitatu, ili wananchi wa maeneo hayo nao waanze kufaidi usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Florens Turuka alisema Bodi yake kwa kushirikiana na Menejimenti ya Wakala itahakikisha mikakati yote na programu za maendeleo ya usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam zinatekelezwa na kusimamiwa kwa ufanisi na umakini wa hali ya juu ili kuwakomboa wananchi na adha ya usafiri.
Aidha Dkt. Turuka alimshukuru Mh. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua kuwa mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, Dkt. Edwin Mhede alisema Wakala utaendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa weledi ili wananchi wa Dar es Salaam wapate huduma bora ya usafiri.
“Tunamshukuru Mh.Rais kwa kutuidhinishia muundo mpya wa Wakala ambao sasa utatupanguvu ya kutekeleza majukumu yetu kwa nguvu zaidi, tunamhakikishia huduma tunayotoa itaendelea kuwa bora na ya uhakika ” Alisema Dkt.Mhede.