Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BODI, DKT. FLORENS MARTIN TURUKA WAKATI WA UZINDUZI WA BODI YA USHAURI YA WIZARA YA WAKALA WA MABASI YAENDAYO HARAKA TAREHE 14 NOVEMBA 2022
19 Feb, 2023 Pakua

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa,

Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB);

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa,

Prof. Riziki Shemdoe;

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya DART;

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART,

Dr. Edwin P. Mhede;

Timu ya Menejimenti ya Wakala;

Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa leo hii tukiwa na afya njema.  Pia nikushukuru na kukupongeza Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kuteuliwa kwako na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa wa Uwaziri katika Wizara kubwa ya  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

 

Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe wapya Bodi ya Ushauri ya Wizara ya DART walioteuliwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dr. Edwin Mhede, Timu ya Menejimenti ya Wakala, Waandishi wa Habari na Wageni wote Waalikwa kwa kuitikia wito wa kujumuika nasi katika halfa hii fupi ya uzinduzi wa Bodi yetu ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka.

 

Mheshimiwa Waziri, Majukumu ya Bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ni kusimamia, kushauri, kubuni mipango na kuhamasisha maendeleo ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Katika Jiji la Dar es Salaam ili kufikia malengo ya kupunguza msongamano katika jiji na kuwawezesha wananchi kufanaya shughuli zao za maendeleo kwa ufanisi zaidi hivyo kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa nchi.  Majukumu mengine ya Bodi ni kuhakikisha wafanyakazi wa DART wanafanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia sheria kanuni na miongozo mbalimbali ya kiutumishi ili kufikia malengo yaliyopangwa ya uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es salaam hivyo, kuharakisha maendeleo ya wananchi kijamii na kiuchumi.

 

Mheshimiwa Waziri, kwa kuzingatia malengo ya wizara yako ya kuhakikisha kunakuwepo na mfumo madhubuti ya usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam, napenda nikuhakikishie kuwa Bodi kupitia uzoefu wa wajumbe walioteuliwa itahakikisha inasimamia uwajibikaji wa Wakala ili iweze kutoa huduma ya usafiri wa umma iliyo bora. Aidha, Bodi itahakikisha inakuwa bega kwa bega na uongozi wa menejimenti ya Wakala  kusaidia utekelezaji wa mikakati ya utekelezwaji wa program zote zilizopo na zinazoendelea ili zikamilike kwa wakati.

 

Mheshimiwa Waziri, Baada ya kusema haya, Napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kukushukuru wewe binafsi na wageni wote waliohudhuria hafla hii. Mwisho nitoe rai kwa uongozi na menejimenti ya DART na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri kufanya kazi kwa ukaribu na weledi ili kuweza kufikia matarajio ya wananchi tunaowatumikia.

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA NA KARIBUNI SANA.