MAELEZO YA KATIBU MKUU, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, PROF. RIZIKI SHEMDOE WAKATI WA UZINDUZI WA BODI YA USHAURI YA WIZARA YA WAKALA WA MABASI YAENDAYO HARAKA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa,
Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB);
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka,
Dkt. Florens Martin Turuka;
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya DART;
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART,
Dr. Edwin P. Mhede;
Timu ya Menejimenti ya Wakala;
Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA;
Ni heshima kubwa kwetu sisi kuwa pamoja siku hii ya leo katika tukio lenye lengo kubwa la kuongeza juhudi na maarifa katika kusimamia Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Jijini Dar es Salaam ambao umepangwa kutekelezwa katika awamu sita.
Awali ya yote, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kukubali mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Kwa niaba ya watendaji wote wa Wizara ya TAMISEMI ningependa kuwakaribisha Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ambayo inazinduliwa leo. Ningependa mjisikie nyumbani mkiwa hapa DART na mnapokuja kikazi katika ofisi za TAMISEMI. Karibuni sana.
Kama mwenyeji ndani ya TAMISEMI, ninajisikia fahari kubwa kuwakaribisha wote kwa ajili ya tukio hili ambalo lina umuhimu wake kwa nchi ya Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, ninachukua nafasi hii kuwashukuru Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ambayo iko chini ya uongozi wa Mtendaji Mkuu, Dr. Edwin Mhede kwa kutukaribisha katika uzinduzi huu wa Bodi ya Ushauri.
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka umefikia mafanikio mengi wakati wa kutekeleza majukumu yake iliyokasimiwa na Serikali katika utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka tangu Wakala huu uundwe, mwanzoni ukiwa chini Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na sasa hivi ukiwa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Hivyo, Wizara mama haina budi kujivunia kuwa na watendaji wenye weledi katika nafasi mbalimbali katika kusimamia miradi ya kimkakati ya maendeleo mojawapo ikiwemo Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
Sote tunafahamu kuwa Dar es Salaam ni moja ya majiji duniani yanayokua kwa kasi. Miaka kumi iliyopita, Dar es Salaam ilikuwa na wakazi takribani Milioni 4. Matokeo ya Sensa na Makazi iliyofanyika Agosti 2022 na kutangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, yameonyesha kuwa Jiji la Dar es Salaam lina wakazi zaidi ya Milioni Tano (Milioni 5). Kutokana na tafiti iliyokwisha fanywa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zinasema kuwa kufikia mwaka 2025, Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na idadi ya watu Milioni 6.2. Ongezeko hili la kasi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam inaonesha ilivyo muhimu kwa Serikali ya Tanzania kuchukua maamuzi ya kuboresha miundombinu mapema iwezekanavyo na kuepuka makosa ambayo yalishakwishafanywa na majiji mengine huko duniani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala, Wajumbe wa Bodi, pamoja na washiriki wote katika uzinduzi huu wa Bodi leo mna fursa nzuri ya kushirikishana mawazo, uzoefu katika kusimamia miradi mbalimbali ya kimkakati na hivyo kuiwezesha Wizara ya TAMISEMI na Tanzania nzima kuleta suluhisho la usafiri wa umma katika majiji makubwa kama Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, wajibu wangu leo ni kutengeneza njia ambapo wewe Mgeni Rasmi utapita katika kutoa mwongozo na maelekezo ya namna Bodi hii ya Ushauri ya Wakala unayoizindua leo itakavyotakiwa kutekeleza majukumu yake katika kutoa ushauri sahihi kwa Wizara.
Mheshimiwa Waziri, uhaba wa miundombinu iliyopitwa na wakati [d1] pamoja na uwepo wa mfumo wa usafiri wa umma ambao umekuwa ukitumia mabasi madogo na pasipo na ratiba maalum kwa muda mrefu unaojulikana kwa jina maarufu la daladala, umesababisha msongamano wa magari katika jiji kila siku na hivyo kuwachelewesha watu wengi kufika kwenye sehemu zao za kazi au biashara hasa kipindi ambacho mradi wa DART ulikuwa haujaanza kutekelezwa katika jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ili kuleta suluhisho la wakazi wa jiji la Dar es Salaam la kuchelewa kufika katika sehemu zao za kazi au biashara kwa [d2] sababu ya msongamano wa magari, Serikali iliamua kuanza kutekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ambao unatumia mabasi makubwa mithili ya treni kwa kutumia njia maalum.
Kwa vile huduma ya usafiri wa umma ni ya muda wote katika jiji kwa siku nzima, kazi ya kusimamia na kuendeleza mradi wa DART ni ya saa zote na kwa siku zote kwa mwaka mzima. Kutokana na umuhimu huu, Serikali imeweka mradi wa DART mojawapo ya vipaumbele katika kuendesha miradi yake ya maendeleo. Kutokana na uzito huo, wewe Mgeni Rasmi upo hapa leo ukiwa mkono wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuzindua Bodi hii.
Pamoja na Bodi hii ya Ushauri kuwa na majukumu yake katika kuishauri Wizara, nina matumaini makubwa leo kuwa utakuwa na msisitizo kwa mambo kadhaa ambayo wewe kama kiongozi mkuu wa Wizara umeona vyema kuifunda Bodi hii kabla haijaanza rasmi kutekeleza majukumu yake.
Kama ilivyo ada katika uongozi wa Awamu ya Sita wa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan ya kuwahimiza viongozi na watumishi wote wa umma kufanya kazi kwa bidii katika taasisi zao ili waweze kuwatumikia wananchi kikamilifu kwa kuacha mazoea ya kila siku, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka hauna budi kufuata falsafa hiyo ikizingatia kujiendesha kwa faida pamoja na kuwa inatoa huduma kwa jamii.
Uteuzi na uzinduzi wa Bodi hii ni juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa Wakala unasimamia mradi wa DART kwa kufuata mikakati mahususi katika kujenga miundombinu na kusimamamia uendeshaji wa huduma ya mabasi.
Mradi wa DART umeshuhudiwa kuwa na mafanikio lukuki katika jiji la Dar es Salaam tangu uanze. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto chache ambazo serikali inaendelea kuzifanyia kazi ikiwemo uhaba wa idadi ya mabasi kwa Awamu ya Kwanza, na kurudisha namna ya kulipa nauli kwa kutumia kadi janja. Tunatambua kuwa Mfumo Mpya wa Kukusanya Nauli umeshaanza kufanya kazi kwa kutumia tiketi zenye alama za utambuzi huku hatua za kuanza kutumia kadi zikiwa katika hatua mbalimbali za manunuzi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka utatekelezwa kwa ufanisi endapo kutakuwa na uongozi wenye maono makubwa. Leo hii kuna Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi hii ya Ushauri ambao leo utawapa vitendea kazi ili wafanye kazi na Menejimenti ya Wakala katika kuufanya mradi wa DART kuwa kichocheo cha mageuzi katika sekta ya usafiri wa umma mijini ndani na nje ya Tanzania.
Baada ya kusema hayo machache, ninachukua fursa hii kumkaribisha Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki azungumze na Bodi teule ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na baadae kuizindua rasmi.
KARIBU SANA MGENI RASMI