Habari
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akiwaongoza Waheshimiwa Wabunge, Watumishi wa Ofisi ya Bunge, pamoja na viongozi mbalimbali katika matembezi wakati wa Azania Bunge Bonanza lilofanyika katika viwanja Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma.

Mashabiki wa Timu ya Simba (Wekundu wa Msimbazi), wameibuka mshindi wa jumla katika Bonanza la Bunge lililofanyika tarehe 1 Februari, 2025 katika Viwanja vya John Merlin Jijini Dodoma.
Bonanza hilo ambalo lilidhaminiwa na Benki ya Azania lilihusisha mashabiki wa Timu ya Simba na Yanga kutoka Ofisi ya Bunge (Waheshimiwa Wabunge na watumishi), watumishi kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) na Wizara ya Maji.
Taasisi nyingine ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF), Chuo cha Mipango Dodoma, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mashabiki wa Timu za Simba na Yanga wa Mkoa wa Dodoma na viongozi wao.
Akitangaza mshindi katika hafla ya chakula cha jioni, Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson alisema katika Bonanza hilo Simba imeibuka mshindi wa jumla kwa kujinyakulia pointi 90 huku Yanga ikiambulia pointi 81.
Baadhi ya michezo ambayo timu za mashabiki wa Simba (mchanganyiko) iliongoza ni pamoja mchezo wa mpira wa miguu, mchezo wa mpira kikapu wanawake, mchezo wa mpira wa wavu wanaume, mchezo wa mpira wa pete wanawake na kuvuta kamba wanawake na wanaume.
Michezo mingine iliyoongoza ni mchezo wa mpira wa meza wanawake na wanaume, mchezo wa ‘draft’ wanawake, mchezo wa kurusha vishale wanaume, mchezo wa ‘pool table’wanawake na wanaume na mchezo wa karata wanawake.
Mheshimiwa Spika aliishukuru Benki ya Azania kwa ushirikiano wao na kwa kudhamini Bunge Bonanza kwa ukubwa wa hali ya juu.
“Azania benki mmetufanya tufurahi, tumefahamiana na watu mbalimbali shukrani kwa kututengenezea fursa hii. “Nawapongeza pia kwa kazi kubwa kuchangia mandeleo ya Nchi, Bunge tunatambua mchango wenu na tunawatakia kila la kheri katika mwaka unaoanza,” alisema.
Aidha, aliwashukukru Waheshimiwa Wabunge, watumishi na washiriki wengine wote kwa ushirikiano waliuonyesha katika Bonanza hilo.
Awali akizungumza katika Viwanja vya John Merlin kabla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa michezo mbalimbali, Mgeni maalum, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alimpongeza Mheshmiwa Spika kwa kubuni wazo la Bunge Bonanza.
Alisema Wazo hilo la kuanzisha Bunge Bonanza linaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza michezo na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Sisi kama Shirikisho tumekuja hapa kwa ajili ya jambo hili muhimu, uwepo wangu nimewawakilisha viongozi wengine wa michezo yote iliyofanyika hapa, nimekuja hapa ili kuonyesha ushindani katika tamasha hili ambalo linashindanisha timu kongwe za jadi, hongereni sana,” alisema.
Alisema TFF inajivunia mafanikio iliyoyapata ambayo yametokana na wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge kwa kuweza kupitisha miswada mbalimbali iliyofanikisha maendeleo ya michezo nchini.
“Bado tunawategemea Mhimili wa Bunge, tunaomba ushirikiano wenu katika mchezo wa mpira wa miguu na michezo mingine,” alisema.
Aidha, aliahidi kushirikiano na Bunge katika ujenzi Shule ya Sekondari ya Wavulana pindi muda utakapofika wa kufanya hivyo katika jambo hilo muhimu kwa jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Mheshimiwa Festo Sanga mbali na kuwashukuru washiriki wote wa Bonanza hilo, alisema dhima yake kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kuhamasisha michezo na kampeni ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Tunatamani kuendelea kulifanya Bonanza hili kuwa moja ya mabonanza kubwa zaidi hapa nchini, tarehe 12 Aprili, 2025 tunakusudia kufanya Bunge Marathon kwa mara ya pili kwa lengo la kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bunge.
Alizishukuru Taasisi mbalimbali na viongozi kutoka timu mbalimbali nchini kwa kuwaunga mkono kwa kushiriki Bonanza hilo lililokuwa na Kauli Mbiu ‘Utani Wetu, Umoja Wetu,’.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Azania,Esther Mang’enya alisema Benki hiyo inathamini umuhimu wa Bunge Bonanza katika kuimarisha afya.
“Sisi tumeona ni muhimu kurudisha faida kwa jamii kwa sababu tunajua umuhimu wa afya, Azania inafanya biashara na wateja wote, wateja wadogo, wateja wa kati na wateja wakubwa, vilevile tunayo akaunti maalum ikiwemo akaunti ya wanawake,” alisema.
Baadhi ya michezo iliyoshindanishwa katika Bonanza ni pamoja na mchezo wa mpira wa miguu, mchezo wa mpira kikapu wanawake na wanaume, mchezo wa mpira wa wavu wanawake, mchezo wa mpira wa pete wanawake na wanaume na kuvuta kamba wanawake na wanaume.
Michezo mingine ni mchezo wa mpira wa meza wanawake na wanaume, mchezo wa ‘draft’ wanawake na wanaume, mchezo wa kurusha vishale wanawake na wanaume, mchezo wa ‘pool table’wanawake na wanaume na wanaume na mchezo wa karata wanawake na wanaume.
Mingine ni mchezo wa kurusha vishale wanawake na wanaume, mbio za mita 100, 1,500, 800 wanawake na wanaume, mchezo wa bao, mchezo wa kurusha tufe wanawake na wanaume, mchezo wa karata wanawake na wanaume, mchezo wa kukimbia na gunia wanawake na wanaume na mchezo wa kukimbiza kuku wanawake na wanaume.
Michezo mingine ni mchezo wa kunywa soda kwa haraka wanawake na wanaume, mchezo wa kula chakula kwa haraka wanawake na wanaume, mchezo wa kupita kwenye pipa wanawake na wanaume, mchezo wa kukimbia na kikombe chenye maji wanawake na wanaume na mchezo wa kuruka kamba wanawake na wanaume.
Mingine ni mchezo wa kupiga danadana wanawake na wanaume, mchezo wa kuvaa soksi wanawake na wanaume, mchezo wa ingia toka wanawake na wanaume na mchezo wa kujaza maji kwenye chupa wanawake na wanaume.