Historia
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilianza mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kabla ya hapo palikuwa na Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) na Bunge la Tanganyika. Vyama viatatu, Tanganyika African National Union (TANU), African National Congress (ANC) na United Tanganyka Party (UTP) vilishiriki uchaguzi wa mwaka 1958 chama kilichoshinda ni TANU iliyopata viti vitano.
Tarehe 19 Machi, 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa Waingereza, Bunge la Uingereza lilipitisha Sheria iliyoitwa The Tanganyika (Legislative Council) Order in Council, 1926 kwa lengo la kuanzisha Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (The Legislative Council of Tanganyika Territory - LEGCO). Baraza hilo lilizinduliwa rasmi Mjini Dar es Salaam tarehe 7 Disemba, 1926.
Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza hilo alikuwa Sir Donald Cameroon aliyekuwa Gavana wa Tanganyika. Wajumbe 20 waliteuliwa na Gavana kuunda Baraza hilo. Sheria zilizotungwa na Baraza zilikuwa zinapelekwa Uingereza ili kupata idhini ya Mfalme. Mwaka 1953, kwa Sheria iliyoitwa The Tanganyika (Legislative Council) Amendment Order in Council, 1953, nafasi ya Spika ilianzishwa kuliongoza Baraza hilo badala ya Mwenyekiti. Spika wa kwanza wa Baraza alikuwa Brigedia William Erick Halstead Scupham.
Kufuatia mabadiliko haya, utaratibu wa kutunga sheria pia ulibadilika ambapo sheria zilizotungwa na Baraza ziliidhinishwa na Gavana kwa niaba ya Malkia wa Uingereza. Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Februari, 1958, Baraza lilipata Wajumbe wa kuchaguliwa, vyama vitatu vya siasa, Tanganyika African National Union (TANU), African National Congress (ANC) na United Tanganyka Party (UTP) vilishiriki ambapo Chama pekee kilichoshinda ni TANU iliyopata viti vitano (5) na kuwa chama cha siasa cha kwanza chenye uwakilishi ndani ya Baraza hilo.
Mwaka 1960 katika uchaguzi ambao ulikuwa sehemu ya maandalizi ya Uhuru wa Tanganyika, Wajumbe wote wa Baraza walikuwa ni wa kuchaguliwa. Kwa upande mwingine, jina la chombo hicho lilibadilika kutoka Baraza la Kutunga Sheria na kuwa Bunge (National Assembly).
Kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 muundo wa Bunge ulibadilika kwa kujumuisha Wabunge kutoka pande zote za Muungano, mwaka 1965 yalifanyika Marekebisho ya Sheria yaliyolifanya Bunge kuwa la chama kimoja. Vilevile, mwaka 1992, Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa (MultiParty System) ulirejeshwa na Bunge likawa la vyama vingi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitia katika mabadiliko ya vipindi mbalimbali toka kuundwa kwa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1926 hadi sasa. Mabadiliko makubwa ya kwanza katika Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1945, yalikuwa ni kuingia kwa waafrika wa kwanza katika Baraza hilo. Gavana alimteua Chifu Abdieli Shangali na Chifu Kidawa Makwaia kuwa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.
Mabadiliko ya pili makubwa yalifanyika mwaka 1953 ambapo Gavana alipoondolewa kuongoza Baraza na nafasi yake kuchukuliwa na Brigedia William Erick Halstead Scupham, aliyeapishwa tarehe 1 Novemba, 1953 kuwa Spika wa kwanza wa Baraza hilo. Kuanzia hapo sheria zilizotungwa na Baraza zilianza kuidhinishwa na Gavana kwa niaba ya Mfalme/Malkia wa Uingereza.
Mabadiliko ya tatu makubwa yalifanyika mwaka 1958 ambapo kwa mara ya kwanza Baraza lilipata Wajumbe wa kuchaguliwa na wananchi. Katika uchaguzi uliofanyika mwaka huo, vyama vitatu vya siasa ambavyo ni Tanganyika African National Union (TANU), United Tanganyika Party (UTP) na African National Congress (ANC) vilishiriki. Chama cha TANU pekee kilishinda katika baadhi ya majimbo na hivyo kukifanya chama hicho kuwa na Wajumbe katika Baraza la LEGCO.
Mabadiliko makubwa ya nne yalitokea mwaka 1960 kwenye uchaguzi wa pili ambao ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya Uhuru wa Tanganyika ambapo Wajumbe wote walichaguliwa. Aidha, jina la chombo hiki lilibadilika kutoka kuwa Baraza la Kutunga Sheria na kuwa Bunge (National Assembly). Lengo lilikuwa ni kuandaa mfumo ili baada ya Uhuru Rais wa Tanganyika awe na Mamlaka Kikatiba ya kutoa idhini kwa sheria zitakazotungwa na Bunge.
Baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 pamekuwa na mabadiliko makubwa mengine matatu. Mabadiliko ya kwanza ni mwaka 1964 ambapo kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bunge lilibadilika na kuwa na sura ya Muungano. Wabunge katika chombo hiki walitoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Mabadiliko ya pili yalifanyika mwaka 1965 ambapo, Katiba ya mpito ilifanyiwa marekebisho kuanzisha utaratibu wa chama kimoja, lengo likiwa ni kuimarisha umoja na amani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabadiliko ya tatu ni kurejea kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa nchini mwaka 1992 ambapo ulilifanya Bunge kuwa la vyama vingi kuanzia mwaka 1995. Aidha, katika kipindi chote kilichopita yamekuwepo mabadiliko madogo madogo ya idadi na aina za Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Histroria ya Maspika tangu mwaka 1953 mpaka sasa;-
S/No. |
SPIKA |
MUDA |
1. |
Mhe. Tulia Ackson, Mb |
Feb. 2022 - Hadi sasa. |
2. |
Mhe.Job Ndugai, Mb |
17 Nov 2015 – Jan. 2022. |
3. |
Mhe. Anne Makinda, Mb |
10 Nov 2010 – 16th Nov 2015 |
4. |
Mhe. Samwel Sitta, Mb |
28 Dec 2005-2010 |
5. |
Mhe. Pius Msekwa, Mb |
28 Apr. 1994 -28 Nov. 2005 |
6. |
Mhe. Chief Erasto A.M. Mang'enya, Mb |
20 Nov, 1973-5 Nov,1975 |
7. |
Mhe. Chief Adam Sapi Mkwawa,M.B.E, O.B.E |
27t Nov, 1962-19 Nov, 1973 6 Nov, 1975- 25 Apr, 1994 |
8. |
A.Y.A.Karimjee,C.B.C |
1 Jan, 1956- 26 Dec, 1962 |
9. |
Sir Barclay Nihill, K.B.E., M.C. |
1 Ma 1958 – 31 Dec, 1958 |
10. |
Brigedia Sir William Scupham, C.M.G, M.C. |
1 November 1953 – 30 Apr, 1958 |