NAIBU WAZIRI ATUNUKU VYETI KWA WASHIRIKI 350, AAHIDI MABORESHO MAKUBWA FETA.
Naibu waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi Ng'wasi Kamani amesema Serikali kupitia wizara yake imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni moja ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).
Bi Kamani amebainisha hayo wakati akitunuku vyeti kwa washiriki 350 waliopata mafunzo juu ya ufugaji samaki kibiashara kwa njia ya vizimba pamoja na uchakataji samaki na uongezaji thamani mazao ya samaki Januari 9,2026.
Amesema kuwa kiasi hiko cha fedha kimetengwa mahususi kwaajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia hususani maeneo ya madarasa, mabweni ya wanafunzi, mabwalo ya chakula pamoja na ofisi za watumishi.
Katika hatua nyingine amebainisha kuwa Wizara imetenga fedha kwaajili ya kununua meli moja ya uvuvi itakayotumiwa na wanafunzi kwenye mafunzo ya uvuvi, magari matatu na vifaa vya kufundishia huku ikiongeza idadi ya watumishi ili kuendana na mahitaji ya sasa ya soko.
Akiongea kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Nazael Madalla amesema kuwa mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kikubwa katika kuimarisha uchumi wa buluu kupitia tasnia ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji sambamba na kuwezesha wanawake na vijana kiuchumi.
Nae Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani amesema kuwa FETA imejipanga kupokea maboresho hayo makubwa na kuanzia Wakala inaendelea kuhuisha mitaala mipya 12 ili kuendana na mahitaji ya sasa ya soko na imejipanga kuanzisha masomo ya shahada ambapo kwa kuanzia itaanza na fani mbili za shahada.
Aidha Meneja wa Kampasi ya Nyegezi Bw Peter Jimmy Masumbuko amebainisha kuwa katika wahitimu 350 waliotunukiwa vyeti hii leo vijana ni 150 na wanawake ni 200 ambapo lengo la mafunzo yao lilikuwa kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa kutoa mafunzo bora yatakayowawezesha kupata ujuzi, kuongeza kipato na kupanua biashara zao.
Pia ametaja mada mbalimbali ambazo washiriki wa mafunzo ya ukuzaji samaki kwa njia ya vizimba wamejifunza kuwa ni Ukuzaji wa samaki kibiashara,Ujasiriamali na masoko, Ukakiki wa ubora wa maji,afya na magonjwa ya samaki, Mifumo ya ukuzaji samaki,uundaji,usimikaji na uhudumiaji wa vizimba, Utengenezaji wa vyakula vya samaki na ulishaji, Uzalishaji wa mbegu za samaki,Uendeshaji wa vyombo vya uvuvi na usalama majini,Udhibiti wa upotevu wa samaki baada ya mavuno na uongezaji thamani pamoja na maadili na utaalamu kazini.
Mada kwa kina mama wasindikaji na wauzaji wa mazao ya uvuvi zilikuwa ni Dhana ya sekta ya uvuvi na fursa za Ujasiriamali, Ushughulikaji safi wa samaki na udhibiti wa ubora, Usindikaji na uhifadhi wa samaki(jadi na kisasa), Ufungashaji,uwekaji lebo na uhifadhi wa bidhaa, Usalama wa chakula,viwango na uhakiki wa bodhaa,Ujasiriamali na usimamizi wa biashara, Masoko na utunzaji kumbukumbu kudigitali pamoja na Usimamizi wa mazingira naatumizi endelevu ya taka za samaki
Kwa upande wake Mwakilishi toka Shirika la maendeleo la Ubelgiji (Enabel) Bw Thomas Aikarua ambao ndio waliodhamini mafunzo hayo kupitia mradi wa Inclu-cities amewataka washiriki waliopata mafunzo hayo kuyatumia kujiletea kipato binafsi na kuongeza pato la Taifa.
Nao washiriki waliopata mafunzo hayo wamesema mafunzo haya yatawasaidia kuongeza ubora wa mazao ya samaki na kuwawezesha kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa huku wakiiomba Serikali kuwawezesha mitaji na kupata soko la uhakika la kuuza bidhaa zao ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao