Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu, ametembelea banda la Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na kuelezwa masuala mbalimbali yanayohusu Baraza hilo.
Mhe. Sangu ameelezwa majukumu yanayotekelezwa na NCC, huduma zinazotolewa na Baraza, pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kwa kutolewa huduma hizo, ambapo alipongeza jitihada zinazofanywa na kusema kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano, pindi itakapohitajika kutoa msaada wa kiutumishi.
Akizungumza baada ya kusikia maelezo hayo, Mhe. Naibu Waziri alisema, NCC ina umuhimu mkubwa kwa taifa, kutokana na majukumu inayoyatekeleza, ikiwemo kuratibu usuluhishi wa migogoro inayohusu sekta ya ujenzi, pamoja na kutoa elimu ya mbinu mbadala za kutatua migogoro kwa wadau wa sekta hiyo na nyingine.
“Awali palikuwa na migogoro mingi katika sekta ya ujenzi nchini, lakini sasa inazidi kupungua. Tunaamini NCC ina mchango mkubwa katika kuipunguza kwa namna yoyote ile inayofanya ikiwemo kutoa mafunzo ya usuluhishi tofauti na mahakama. Tunatambua hili na tunapongeza jitihada hizi,”Naibu Waziri Sangu amesema.
Amesema, uwepo wa NCC umeleta uwiano wa mambo mengi katika sekta ya ujenzi nchini.
Kuhusu ushiriki wa NCC kwenye Wiki ya Utumishi wa Umma
Naibu Waziri Sangu ameitaka NCC izidishe ushiriki wake kwenye matukio mengi Zaidi, kama ilivyo shikiri kwenye wiki ya Utumishi wa umma ili watanzania waifahamu zaidi na kuitumia.
Amesema, majukumu yake ni makubwa na ya msingi yanayopaswa kutangazwa zaidi ili yajulikane kwa jamii yote na wala si kwa makandarasi au wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi pekee.
“Tumefurahia maandalizi ya banda lenu na ushiriki wenu katika wiki hii muhimu. NCC imeonesha utayari wa kuhudumia wananchi hivyo, Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaahidi kuwaunga mkono,”
Banda la NCC limetembelewa na viongozi mbalimbali kwa siku tofauti, akiwemo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (UTUMISHI) Bw.Juma Mkomi, pamoja na Mkurugenzi wa ofisi hiyo, Bw. Benard Makhanda, Mkurugenzi Msaidizi wa UTUMISHI, Bw. Jafari Maganga na wengine wenye nyadhifa tofauti, walioambatana nao.