Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Ujenzi

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI

Huduma Zetu

HUDUMA ZETU

1. Mafunzo

Mafunzo yatolewayo na baraza yanalenga kuboresha uwezo na utendaji wa watendaji katika Sekta ya Ujenzi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Mafunzo hayo husaidia katika upatikanaji wa mbinu bora zinazohitajika katika uboreshaji wa huduma, hivyo kuimarisha ushindani na kuhakikisha thamani ya pesa kwenye miradi inayojengwa.

Baraza linaendelea kutekeleza mipango kadhaa ya mafunzo kwa vitendo. Maeneo mahususi yanayozingatiwa ni pamoja na: Manunuzi ya Umma, Usimamizi wa Mikataba na Miradi ya Ujenzi, Makadirio ya Gharama za Ujenzi, Kaguzi za Kiufundi, Usuluhishi wa Migogoro katika utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi (Usuluhisi nje ya Mahakama), Madai katika Miradi ya Ujenzi, Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Teknolojia ya nguvu kazi katika ukarabati wa Barabara, Ukarabati wa Majengo.

Baraza pia huendesha mafunzo kulingana na huitaji wa wateja.

Mafunzo yatolewayo na Baraza hulenga washiriki kutoka fani mbalimbali zikiwemo:  Wahandisi, Wasanifu Majengo, Wakadiriaji Majenzi, Wathamini, Wasimamizi wa Majengo, Wataalamu wa Bima,  Wahasibu, Wanasheria, Wakadiriaji Vipimo, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Maafisa Mipango, Washauri Elekezi na Mafundi.

 2. Usuluhishi wa Migogoro

Tangu mwaka 1982 Baraza limekuwa likiratibu migogoro katika sekta ya ujenzi kwa njia ya usuluhishi. Baraza limeandaa orodha ya Wasuluhishi wa migogoro katika sekta ya ujenzi ambao husajiliwa na kutumiwa na wadau kwaajili ya usuluhishi wa migogoro inayojitokeza katika sekta. Aidha, utatuzi wa migogoro hufuata miongozo ya usuluhishi ambayo imechapishwa na Baraza.

3. Kaguzi wa Kiufundi

Madhumuni ya kufanya ukaguzi wa kiufundi katika miradi ya ujenzi ni kuwasaidia wawekezaji/watoa fedha kupata maelezo kuhusu mwenendo na utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na mapungufu yaliyopo na utatuzi wake.

Ukaguzi unaweza kufanyika katika hatua yoyote ya mradi ikiwa ni pamoja na matayarisho ya utekelezaji, wakati wa utekelezaji na baada ya mradi kutekelezwa. Baraza limekuwa likitoa huduma hii kwa serikali na taasisi zake na sekta binafsi.

4. Huduma za Ushauri

Baraza linashughulika na kutoa ushauri wa kiufundi katika mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi; ikiwa ni pamoja na: mipango kuhusu utekelezaji wa miradi, ununuzi na usimamizi wa mikataba ya ujenzi, usimamizi wa gharama za miradi na ukaguzi wa miradi.

5. Uratibu wa Sekta ya Ujenzi

    5.1 Sera na Mikakati

Baraza limehusika katika uratibu na uundaji wa sera na mikakati mbalimbali kwa ajili ya sekta ya ujenzi kama ifuatavyo:

  • Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Ujenzi wa mwaka 1991
  • Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2003;
  • Mpango wa Utekelezaji wa Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2006.
  • Mwongozo wa ununuzi unaohusisha utekelezaji wa miradi kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa mwaka 2008;
  • Rasimu ya Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi ya mwaka 2008
  • Mapitio ya Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2017.

5.2 Vyama na Bodi za Usajili

Baraza lilihamasisha uundwaji wa bodi za usajili na vyama vya wadau wa Sekta ya Ujenzi ;ikiwa ni pamoja na:

  • Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB);
  • Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB);
  • Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB);
  • Chama cha Wabunifu Majengo (AAT);
  • Chama cha Wahandisi Washauri (ACET);
  • Chama cha Makandarasi wa Ujenzi (TACECA);
  • Chama cha Barabara (TARA).
  • Taasisi ya Usuluhishi na Migogoro (TIArb);
  • Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi (TIQS);
  • Chama cha Wajenzi wa Sekta isiyo Rasmi (TAICO);
  • Mfuko wa Maendeleo wa Sekta ya Ujenzi (CIDF);

5.3 Makongamano ya Sekta ya Ujenzi

Kuanzia mwaka 2001, Baraza limekuwa likiandaa makongamano ya sekta ya ujenzi kila baada ya miaka miwili. Madhumuni ya makongamano ya Sekta ya Ujenzi ni kusaidia upangaji, uratibu pamoja na kuboresha maendeleo ya Sekta ya Ujenzi kwa kuzingatia yafuatayo:

  • Dira, malengo na mikakati ya maendeleo ya sekta ya ujenzi;
  • Mikakati ya kukuza uwezo ili kuboresha utendaji katika sekta;
  • Ukuaji wa sekta ili kukabiliana na ushindani wa Kimataifa;
  • Uhusiano wa kimataifa.

6. Utafiti

Kazi za utafiti zinazolenga katika kutambua matatizo mbalimbali na ufumbuzi wake yanayohusiana na sekta ya ujenzi kwa ujumla, ni mojawapo ya shughuli za Baraza. Tafiti zilizowahi kufanywa na Baraza ni pamoja na:

Tafiti kuhusu uanzishwaji wa mfuko maalum wa kuwasaidia wadau wa sekta ya ujenzi kupata mahali pa kukopa fedha au kupata dhamana kwa ajili ya miradi ya ujenzi;

  • Mahitaji ya mafunzo kwa washauri elekezi wazawa katika uhandisi wa barabara;
  • Mahitaji ya rasilimali watu katika sekta ya ujenzi nchini Tanzania;
  • Mahitaji ya mafunzo kwa washauri na wakandarasi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kilimo;
  • Uanzishwaji wa mfuko endelevu wa mafunzo kwa wadau wa sekta ya ujenzi nchini;
  • Mapendekezo ya kuhuishwa sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Ujenzi;
  • Utafiti kuhusu namna ya kuliwezesha kifedha, Baraza la Taifa la Ujenzi ili kuweza kutekeleza majukumu yake;
  • Utafiti kuhusu ajira katika miradi mikubwa nchini;
  • Mapitio ya kitaasisi na kisheria kutoka kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi nchini;
  • Utafiti kuhusu wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi katika ujenzi.