Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Ujenzi

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI

Kuhusu sisi

KUHUSU SISI

Utangulizi:

Baraza la Taifa la Ujenzi ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge namba 20 ya mwaka 1979 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008. (“National Construction Council Act, CAP 162, R.E. 2008”). Baraza lilianzishwa kwa lengo la kusimamia maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

Sisi ni nani:

Sisi ni taasisi ya Serikali yenye mamlaka ya kuendeleza sekta ya ujenzi nchini. Katika kutekeleza azma hiyo, tunazingatia mahitaji yote yanayokusudiwa kubadilisha sekta kupitia uwekezaji wa teknolojia ya kisasa. Kwa sasa, Baraza linashughulikia uratibu na uandaaji wa nyaraka zifuatazo:

  • Sera ya Sekta ya Ujenzi (CIP);
  • Sheria ya Majengo Tanzania;
  • Kanuni za Majenzi Tanzania;
  • Viwango vya Majengo na Samani za Serikali;
  • Uratibu wa Maudhui ya Ndani ya Sekta ya Ujenzi;
  • Viwango msawazo vya  Majengo na Samani za Serikali.

 Tunu za Taasisi

Katika kutekeleza dira, dhima na majukumu yake, Baraza linaongozwa na tunu zifuatazo:

  • Huduma Bora
  • Uadilifu
  • Ushirikiano
  • Ubunifu
  • Weledi
  • Uwazi
  • Uwajibikaji

Majukumu

  • Kuhamasisha na kuweka mikakati ya kukuza, kuendeleza na kupanua Sekta ya Ujenzi nchini Tanzania husasan kwa kujenga uwezo na ushindani wa wazawa ili waweze kushindana na kutekeleza miradi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi;
  • Kushauri Serikali juu ya maendeleo ya Sekta ya Ujenzi nchini na kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wa ushauri huo;
  • Kutoa ushauri na msaada wa kitaalamu kwa wadau wa Sekta ya Ujenzi nchini kuhusu mambo yanayohusiana na sekta ya ujenzi;
  • Kuratibu na kuendeleza mafunzo bora kwa wote wanaojihusisha au wanaotarajia kujihusisha na shughuli za ujenzi na shughuli nyingine katika Sekta ya Ujenzi nchini;
  • Kufanya, kuhimiza na kuratibu utafiti katika shughuli zote za Sekta ya Ujenzi;
  • Kuhamasisha, kukusanya, kuchakata na kuchapisha taarifa mbalimbali zinazohusu Sekta ya Ujenzi;
  • Kuhamasisha na kufuatilia uandaaji na utumiaji wa viwango vya ubora, kanuni na miongozo mbalimbali inayohusiana na shughuli za Sekta ya Ujenzi nchini;
  • Kuhamasisha, kushawishi, kubuni na kutumia teknolojia bora na mbinu bora za utendaji katika Sekta ya Ujenzi nchini;
  • Kuhamasisha na kuanzisha majukwaa ili kuratibu shughuli za wadau wa Sekta ya Ujenzi na kuwezesha kushirikiana na kujadiliana katika masuala yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Ujenzi nchini;
  • Kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Sekta ya Ujenzi nchini;
  • Kutafuta na kusimamia fedha za mafunzo ya wataalum na mafundi katika Sekta ya Ujenzi;
  • Kuhamasisha ubora katika sekta ya ujenzi, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya ujenzi;
  • Kuhamasisha mbinu za ujenzi zenye kuzingatia uhifadhi endelevu wa mazingira pamoja na afya na usalama wa kazi katika shughuli za ujenzi;
  • Kuhamasisha kuuza nje bidhaa na huduma za sekta ya ujenzi; na
  • Kuratibu na kuwezesha utatuzi wa migogoro inayotokea katika miradi ya ujenzi kwa ufanisi.

  Kanuni

  • Kutambua na kukubali wajibu wetu kwa taifa wa kuhakikisha kuwa miradi ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi inaendelezwa na kudumishwa kwa ufanisi ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
  • Kutoa miongozo, uwajibikaji na uwezo kwa tasnia, katika kuhakikisha ufanisi na uchumi vinapatikana.
  • Kutoa huduma bora kwa wateja kwa ufanisi.
  • Kujiendeleza kiteknolojia katika kutoa huduma bora.
  • Kuongeza ujuzi na uzoefu kwa wafanyakazi wetu kupitia mafunzo mbalimbali
  • Kuwapatia wadau wa sekta ya ujenzi fursa sawa katika kutekeleza majukumu yao.