Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Ujenzi

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI

Habari

‘Mafunzo yanayoendeshwa na NCC yanatujenga’


image title here


WADAU wa Sekta ya Ujenzi wanaoshiriki mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), wamesema mafunzo hayo yana faida kubwa kwa wengi, kwa sababu yanawajenga kwa kuongeza uelewa wao, hivyo kuchochea weledi wao kazini.

Wamesema, kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi walio katika sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ya ujenzi, wanashauri waajiri au watendaji katika taasisi, mashirika na hata vyama vya kisekta, wayape kipaumbele kwa kuruhusu ushiriki wa watumishi wao wengi zaidi katika mafunzo hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo kuhusu Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi (Course on Construction Contract Administration) jijini Mwanza hivi karibuni, washiriki hao wamesema uelewa wa masuala ya usimamizi wa mikataba ya ujenzi walionao baada ya mafunzo hayo ni tofauti na waliokuwa nao awali.

Miongoni mwao ni Meneja Miliki kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD), Deo Francis Orauya anayeeleza mategemeo yake baada ya kupata mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kuiletea MSD matokeo mazuri zaidi katika maeneo mawili; usimamiziwa mikataba ya ujenzi na uhusiano mzuri kati ya MSD na wahusika wengine wa mikataba ya ujenzi wa maghala ya bohari ya dawa.

Anasema, “Kwa namna nilivyofaidika na kupata uelewa zaidi kuhusu usimamizi bora wa mikataba ya ujenzi, ninashauri taasisi nyingine, mashirika ya umma na ya binafsi yaruhusu idadi kubwa zaidi ya watumishi wao kushiriki mafunzo mbalimbali yanayotolewa na NCC kwa sababu yana faida”.

Kwa upande wake, Mhandisi Mohamed Nahodha Mohamed kutoka taasisi ya Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), anasema itakuwa heri kwa Serikali na wananchi kwa ujumla, ikiwa watendaji na maofisa wa ngazi mbalimbali wengi zaidi watapata mafunzo yanayotolewa na Baraza la Taifa la Ujenzi kulingana na mahitaji ya taasisi zao.

Mhandisi Mohamed anasema kabla ya kupata mafunzo kuhusu usimamizi wa mikataba ya ujenzi, alikuwa na maswali mengi yanayomtatiza, ambayo yaligeuka kuwa changamoto ngumu kwake.

“…Lakini sasa nimekwishakuwa Mhandisi Mshauri mwenye uelewa mpana kuhusu masuala ya usimamizi wa miradi tofauti na ilivyokuwa awali. Nitatumia maarifa na uelewa nilioupata kutoka katika mafunzo haya kuiletea tija taasisi ninapofanya kazi, ambayo, kwa kuipitia, wananchi nao watafaidika.

Naye Mhandisi Julius Mamiro aliyehusika kutoa mafunzo hayo kwa niaba ya NCC anasema ushiriki wa wengi zaidi unaleta mafanikiozaidi kwa sababu uelewa hautakuwa kwa mtu mmoja mmoja bali kwa wengi wanaoshiriki kutekeleza shughuli fulani ya taasisi yao au kusimamia mradi.

Anasema kutokana na hilo, anaamini kuharibu mradi au kazi na kuleta hasara kwa taasisi, serikali au kampuni haitakuwa jambo la kutegemewa.

“Watumishi wengi wakiwa na uelewa mpana kuhusu jambo fulani, wanaweza kulitekeleza kwa wepesi, haraka na kwa ufanisi kuliko wasio na uelewa mpana.

Kutokana na hili, ninashauri Serikali na taasisi zake, mashirika ya umma na ya binafsi na hata watu mmoja mmoja wahudhurie mafunzo ya NCC kwa sababu yanafaida kubwa,”Mamiro anasema.