Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI ATEMBELEA TBA

Imewekwa: 18 September, 2024
NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI ATEMBELEA TBA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde ametembelea Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kukutana na Menejimenti katika Ofisi ndogo za TBA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Dkt. Msonde amepokea wasilisho juu ya Majukumu ya TBA, mafanikio, changamoto na utatuzi wake. 
Baada ya wasilisho na kutembelea miradi inayotekelezwa na TBA jijini Dar es Salaam, Dkt. Msonde amesema ameridhishwa na namna TBA inavyotekeleza majukumu yake katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kutoa maekelezo kwa lengo ya kuchochea ufanisi na utendaji kazi.

Akizungumza wakati wa Ziara hiyo Dkt. Msonde amesema amefurahishwa na kazi nzuri inayotekelezwa na TBA hasa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikijumuisha ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na miradi ya mingine ambayo TBA inapewa jukumu na Serikali.

"Mmefanya kazi nzuri sana katika Jengo la Ofisi ya Rais Utumishi. Lile jengo limejengwa kisasa na nilipoambiwa kazi ile imefanywa na TBA nilistaajabu kwa sababu ujenzi umekamilika kwa wakati na mmefanikiwa kuweka miundombinu ya kisasa ambayo ni kivutio kwa Mji wetu wa Serikali" amesema Dkt. Msonda.

Pia Msonde ameitaka TBA kuhakikisha inakuja na mpango madhubuti wa kutatua changamoto ya makazi ambapo amesema uhitaji wa makazi bora unaongezeka kwa kasi ikilinganishwa na idadi ndogo ya nyumba zinazojengwa.

Vile vile ameitaka TBA kudumisha ushirikiano kati ya viongozi na viongozi, viongozi na watumishi, TBA na Taasisi nyingine zilizopo ndani ya Wizara ya Ujenzi na ushirikiano kati yake na Wizara ya Ujenzi. kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi kwa maendeleo ya Wizara kwa ujumla.

Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa TBA fedha kwa ajili ya kuboresha makazi na kuchochea uchumi nchini.