MENEJIMENTI YA TBA YAHIMIZWA KUKUTANA MARA KWA MARA.
Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeaswa kukutana mara kwa mara na kufanya vikao vya tathmini ya utendaji kazi. Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti ya TBA. Akizungumza katika Kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Qs. Mwanahamisi Kitogo amesema vikao hivyo vina umuhimu mkubwa kwa Menejimenti ya TBA kwakuwa vinaboresha utendaji kazi.
"Vikao kazi hivi (retreat sessions) ni vyema vikawa endelevu kwa kuwa vinasaidia Wakala kujitathimi kwa kujipima utendaji kazi na ufanisi wa malengo yaliyowekwa katika kutekeleza Sera na maelekezo ya Serikali kwa ujumla".
Pia amewataka wafanyakazi wa TBA kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Serikali ya kutumia kila siku mfumo wa upimaji wa utendaji kazi (PEPMIS/PIPMIS) kwa lengo kuongeza ufanisi wa majukumu ya Wakala.
Awali akizungumza katika Kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro alisema Kikao kazi hicho kina lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya TBA. Pia amesema kupitia Kikao hicho wanakwenda kujadili na kujifunza mambo mbalimbali kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya TBA kwa weledi, umakini, uadilifu na kujali maslahi ya umma kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Menejimenti ya TBA inakutana kufanya kikao kazi cha siku mbili (2) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa majukumu ya TBA katika Ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.