MHE. BASHUNGWA AZINDUA NYUMBA ZA MAKAZI YA WATUMISHI WA UMMA ZILIZOJENGWA ENEO LA MAGOMENI KOTA AWAMU YA PILI
Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha nyumba za makazi zinazosimamia wapangaji wote wanalipa kodi kwa wakati pamoja na kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu kwa kufata sheria za mikataba ili fedha hizo zitumike katika ujenzi wa majengo mawili kwa ajili ya watumishi wa Umma (Block C na D,) Magomeni Kota awamu ya pili ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 15.
Akizungumza leo Julai 23, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya Ufunguzi wa Nyumba za Makazi zilizojengwa na TBA katika eneo la Magomeni Kota Awamu ya pili ‘B’ lililogharimu shilingi Bilioni 5.6 Mhe. Bashungwa amesema kuwa Serikali imeendelea na jitihada za kujenga makazi bora kwa watumishi ili kupunguza changamoto za makazi.
Amesema kuwa na watumishi waliopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo kutimiza wajibu kwa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha TBA kujenga nyumba nyingi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa uhitaji wa nyumba bora umefikia zaidi ya nyumba milioni tatu kwa ongezeko la nyumba laki tatu na tisini elfu kila mwaka.
Ameelekeza Wakala hiyo kuendelea kufanya kazi kiwango bora na ubunifu zaidi kwa wakati huu ambao Serikali imerekebisha sheria ya Wakala kwa kutoa fursa kwa TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na Taasisi za fedha katika uendelezaji milki, kujenga nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma pamoja na watanzania kwa ujumla.
Aidha ameipongeza Wakala hiyo kwa kuwa wabunifu katika ardhi na mipango ya majengo ya kisasa katika miradi wanayoisimamia, ambapo katika eneo la Magomeni lenye hekari 32 awali lilikuwa na wakazi 645 na baada ya TBA kusimamia ujenzi na ukadiriaji majengo ekari 9 zimejengwa nyumba za makazi zilizotosheleza wakazi 645.
“TBA inakwenda katika mwelekeo sahihi katika ubora wa majengo pamoja na teknolojia ikiwemo hii ya kitasa janja itakayosaidia kuwadhibiti wanaokwepa kulipa kodi…..TBA chukueni hatua kwa wadaiwa sugu bila kuangalia wadhifa.” Ameongeza Bashungwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema mradi huo umegharamiwa na Serikali kwa fedha za ruzuku zipatazo shilingi Bilioni 5.687 na utekelezaji wake ulianza Novemba 2022.
Amesema jengo hilo ni la pili kati ya majengo 5 yanayojengwa katika eneo hilo kwa ajili ya makazi ya watumishi wa Umma ambapo jengo moja tayari limekamilika na limepangishwa na hadi kukamilika kwa majengo yote matano jumla ya kaya 80 zitakuwa zikiishi hapo, Na ujenzi wake umezingatia kanuni na misingi ya ujenzi wa majengo ya Serikali.
“Jengo A limekamilika na tayari limepangishwa, jengo B ni hili ulilolizindua leo na majengo mawili C na D ujenzi wake umefikia asilimia 15 na ukamilishaji wa majengo hayo yaliyosalia kadiri ya mpango kabambe uliopo utategemea upatinaji wa fedha.” Amesema.
Kuhusiana na ubunifu unaofanywa na Wakala hiyo Kondoro amesema; ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) ya 2020/2025 ibara ya 55 (h) inayoelekeza maeneo yaliyorejeshwa Serikali Kuu chini ya Wakala hiyo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelezwa kwa kujenga nyumba zinazoweza kubeba familia nyingi (apartments.) bora na za kisasa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema, uzinduzi huo ni matokeo mazuri ya utendaji kazi TBA chini ya Wizara ya Ujenzi ambao wamekuwa wakitekeleza miradi kwa teknolojia ya ubora na upangaji wa miji.
“Nyumba hizi msiwape wahuni, wanaofanya kazi ya udalali na baadaye kuleta taharuki za madai ya kodi kubwa na gharama nyingine na kuharibu taswira ya eneo hili, nyumba hizi zinapangishwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kodi ya soko.” amesema.