Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

NAIBU WAZIRI KASEKENYA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Imewekwa: 28 February, 2025
NAIBU WAZIRI KASEKENYA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI

MOROGORO - Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya amefungua Mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega. Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Mhe. Kasekenya ametoa pongezi kwako Mwenyekiti wa Baraza kwa kutambua umuhimu wa kuijenga na kuiimarisha TBA kwa njia ya ushirikishaji wa wafanyakazi kwenye shughuli za Wakala kupitia Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi. Pia ameyataka Mabaraza kuwa na tija kwa kutoa ushauri kwa waajiri juu ya namna bora ya kuongeza ufanisi na tija katika maeneo ya kazi.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa viongozi na wafanyakazi kuendelea kutumia mfumo huu kushauri namna bora ya kuboresha utendaji. Hata hivyo, vyama vya wafanyakazi visitumike kuwa vyanzo vya kuchochea migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu kazini” ameongeza Mhe. Kasekenya.

Aidha, akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mkurugenzi wa Rasilimali na Utawala wa Wizara ya Ujenzi Bw. Mrisho Mrisho amepongeza kazi kubwa inayofanywa na TBA katika maeneo mbalimbali hapa nchini. “Wizara inathamini na kutambua mchango wa TBA katika utekelezaji wa majukumu yenu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuhakikisha watanzania na watumishi kwa ujumla wanakuwa na makazi ya uhakika na kutoa huduma za ushauri katika masuala yanayohusu ujenzi” amesema Bw. Mrisho.

Pia Katibu Mkuu anawapongeza kwa ushiriki mzuri kwenye miradi mbalimbali ambayo TBA imekuwa ikiisimia ikiwemo ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Utumishi, Ofisi ya Rais, Ikulu Dodoma na mradi wa nyumba 300 za Nzuguni ambazo tayari watumishi wameshaanza kuingia ameongeza Bw. Mrisho.

Awali akitoa salamu, Mwenyekiti wa Baraza na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro alizitaja baadhi ya agenda zitakazojadiliwa katika Mkutano huo kuwa ni pamoja na Kupokea na kujadili utekelezaji wa bajeti ya Wakala kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na kuwasilisha rasimu ya Bajeti ya Wakala kwa mwaka 2025/2026 na Uombaji wa miradi katika mfumo wa manunuzi (NeST).