TBA NA ZBA KUENDELEZA MASHIRIKIANO
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kuendelea kushirikiana kufuatia Hati ya Makubaliano ya Mashirikiano iliyosainiwa Novemba 21, 2023.
Akizungumza baada ya kikao hicho Mtendaji Mkuu wa ZBA Mha. Kassim A. Omary amesema kikao hicho ni matokeo ya hati hiyo ya makubaliano ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu walioelekeza taasisi zinazofanya kazi zinazofanana Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana.
Mha. Kassim amesema kuwa kikao hicho kimekuwa na manufaa makubwa ambapo kamati ya wataalamu kutoka TBA na ZBA yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa maswala ya ushirikiano imeundwa na inatarajia kuanza kazi rasmi Januari 22, 2025.
Vile vile Mha. Omary amebainisha manufaa yanayotarajiwa kutokana na ushirikiano huo kuwa ni pamoja na kuharakisha utekelezaji wa majukumu kwa pande zote.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amesema ushirikiano huo utawezesha wataalamu wa TBA na ZBA kubadilishana uzoefu, kujifunza kutokana na kazi mbalimbali zinazotekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar, kupeana fursa za mafunzo ya ndani na nje ya nchi pamoja na kufanya tafiti.
Kikao hicho kiliambatana na ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TBA Mkoa wa Dar es Salaam katika maeneo ya Canadian Masaki na Magomeni Kota pamoja na kutembelea Kiwanda cha kuzalisha malighafi za ujenzi kama tofali na zege.