TBA YAFANYA UKAGUZI WA VIWANJA VYAKE MKOA WA PWANI
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ukiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Miliki, FRV. Said Mndeme (ndc) umefanya ziara ya kukagua na kufuatilia viwanja vyake vilivyopo katika maeneo ya Simbani Mwendapole, Kibaha na Chalinze mkoani Pwani.
Ziara hiyo iliyofanyika leo Oktoba 24, 2025 imelenga kuhakikisha usimamizi bora wa mali za serikali pamoja na kutambua changamoto zinazohitaji suluhisho la haraka katika maeneo hayo.
Akizungumza ofisini kwake alipokutana na ujumbe wa TBA, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Aboubakar Kunenge, amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo sekta ya makazi na biashara.
“Nawakaribisha TBA kuwekeza zaidi katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara mkoani Pwani. Tunazo fursa nyingi na mali ghafi hupatikana kwa bei nafuu,” amesema Mhe. Kunenge.
Kwa upande wake, FRV. Mndeme amesema TBA itaendelea na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miliki zote za wakala huo nchini ili kuhakikisha zinatunzwa ipasavyo.
Aidha, ametoa onyo kwa wananchi wanaovamia maeneo yaliyotengwa na serikali, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
“TBA haitasita kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya serikali bila kibali. Ni muhimu wananchi waheshimu mipaka na taratibu zilizowekwa,” amesisitiza FRV. Mndeme.
Ziara hiyo ni muendelezo wa ukaguzi wa maeneo yanayomilikiwa na TBA katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na kuandaa mikakati ya kuyaendeleza.