TBA YAKABIDHI JENGO LA OFISI ZA HAZINA MKOANI GEITA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekabidhi rasmi jengo la Ofisi za Hazina ndogo mkoani Geita kwa Wizara ya Fedha katika hafla iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo.
Akizungumza katika Hafla hiyo iliyofanyika Bombambili mjini Geita Mhe. Nyongo amesema kuwa jengo hilo litaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, taasisi za umma na binafsi, na kuondoa adha ya wananchi wa Geita kufuata huduma nje ya mkoa.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Bi. Amina Lumuli, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kukamilisha mradi huo.
Aidha, Bi. Lumuli ameeleza kuwa uwepo wa jengo hilo lenye miundombinu ya kisasa kutaongeza ufanisi wa utendaji, kuimarisha usalama wa taarifa na mali, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi pamoja na kuonyesha utayari wa kushirikiana kutekeleza miradi mingine. "TBA ipo tayari kushirikiana na Wizara yako katika utekelezaji wa miradi mingine katika maeneo mbalimbali nchini" aliongeza Bi. Lumuli.
Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Hazina ndogo Mkoani Geita umetekelezwa kwa muda wa miezi 15 chini ya Mkandarasi Masasi Construction Co. Ltd na kusimamiwa na TBA kama Mshauri Elekezi.