Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAPONGEZWA KWA UJENZI WA NYUMBA ZA MAKAZI NZUGUNI

Imewekwa: 13 March, 2025
TBA YAPONGEZWA KWA UJENZI WA NYUMBA ZA MAKAZI NZUGUNI

Dodoma – Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 3,500 za makazi katika eneo la Nzuguni, jijini Dodoma.

Kamati hiyo imetoa pongezi hizo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambao kwa sasa uko katika awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 60 za chinu na nyumba 90 za ghorofa. Tayari nyumba 150 za awamu ya kwanza zimekamilika na zinatumika kwa makazi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustine Vuma (Mb), amesema mradi huo umebuniwa kwa ubunifu wa hali ya juu na unatekelezwa kwa viwango vinavyoridhisha. Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha nyumba hizo zinatunzwa vizuri ili zidumu kwa muda mrefu.

“Tumeona kazi nzuri iliyofanyika, ni mradi mzuri unaovutia. Tunashauri TBA kushirikiana na taasisi kama TARURA ili kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya mradi huu kwa kiwango cha lami,” amesema Mhe. Vuma.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daudi Kondoro, amesema TBA itaingia ubia na sekta binafsi ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi. Amebainisha kuwa TBA tayari imesaini makubaliano na wawekezaji kutoka nje ambao watashiriki katika awamu ya pili ya mradi.

“Mbali na kushirikiana na sekta binafsi, tunapunguza gharama za ujenzi kwa kuwa na kiwanda cha kuchakata zege hapa Nzuguni,” amesema Arch. Kondoro.

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu na utakapokamilika utajumuisha huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo shule, zahanati, maeneo ya kucheza na maeneo ya kupumzika.