TBA YAWAPATIA WATUMISHI WAPYA MAFUNZO ELEKEZI

Watumishi wapya 15 wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wameanza mafunzo elekezi rasmi leo Februari 17, 2025, yaliyofunguliwa na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro. Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Akiba jijini Dar es Salaam na yanatolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC).
Arch. Kondoro aliwakaribisha watumishi wapya na kusema kuwa mafunzo hayo yatatoa fursa ya kujifunza masuala muhimu kutoka kwa wataalamu mbalimbali. Aliongeza kuwa TPSC itahakikisha watumishi wanapata ujuzi wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kufuata miongozo ya Utumishi wa Umma.
Pia, Arch. Kondoro alisisitiza kuwa baada ya mafunzo, watumishi wataendelea kupimwa ili kuhakikisha kwamba ujuzi uliopatikana unaleta mabadiliko chanya katika utekelezaji wa majukumu ya TBA. Mafunzo elekezi kwa watumishi wapya ni matakwa ya kisheria katika Utumishi wa Umma, ambapo inategemea Kanuni G. 1(8) za Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 4 wa mwaka 2005, unaozungumzia umuhimu wa kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya.