Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

WANAWAKE TBA WASHIRIKI KONGAMANO LA WANAWAKE JIJINI ARUSHA

Imewekwa: 13 March, 2025
WANAWAKE TBA WASHIRIKI KONGAMANO LA WANAWAKE JIJINI ARUSHA

Wanawake wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wameshiriki kongamano la wanawake lililofanyika Machi 6, 2025, jijini Arusha, kama sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka. Kongamano hilo ambalo limelenga kuhamasisha wanawake kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na kuhamasisha ushirikiano kati ya wanawake na wanaume katika nyanja mbalimbali, limefunguliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stagomena Tax.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Dkt. Stagomena amesisitiza umuhimu wa wanawake kuzitendea haki nafasi wanazopata na kuhimiza asasi za kiraia kutoa fursa sawa. Aidha, amesisitiza ushirikiano wa wanawake na wanaume katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia yatafanyika Kitaifa jijini Arusha na kuongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Kauli mbiu isemayo "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji".