Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

WATUMISHI WAPYA WAASWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Imewekwa: 28 February, 2025
WATUMISHI WAPYA WAASWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Watumishi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wameaswa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, kanuni, sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Ujenzi TBA Arch. Wencelaus Kizaba wakati akifunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 15 wa TBA yaliyofanyika kwa muda wa siku 5 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam.

"Ninawashukuru sana washiriki wote kwa jinsi mlivyoonyesha utulivu mkubwa na michango mbalimbali ambayo mmeitoa kwa siku zote mlizohudhuria mafunzo haya. Mmeonyesha ukomavu na kiu ya kupata mafunzo kama haya na mengineyo. Niwaombe washiriki wote tukaoneshe kwamba tumetoka kwenye mafunzo kwa kufanya kazi zetu kwa kuzingatia maadili, kanuni, sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma” amesema Ach. Kizaba.

Aidha, Arch. Kizaba amesema kuwa ana imani mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi wapya yatakwenda kuongeza tija na kuwa msaada mkubwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu katika ofisi za TBA.

Mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya ni utekelezaji wa twaka la kisheria katika Utumishi wa Umma ambapo imeelekezwa kwenye miongozo mbalimbali ndani ya Utumishi wa Umma na kwa mujibu wa Kanuni G. 1(8) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi na. 4 wa Mwaka 2005 ambapo unaeleza umuhimu wa kutolewa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya.