Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

WAZIRI ULEGA AKUTANA NA TAASISI ZA UJENZI

Imewekwa: 07 May, 2025
WAZIRI ULEGA AKUTANA NA TAASISI ZA UJENZI

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), amekutana na viongozi na watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi mara baada ya kupitishwa kwa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Kikao hicho kimelenga kuhimiza utekelezaji wenye tija wa bajeti ya trilioni 2.28, huku akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya Taasisi na Wizara.

Mhe. Ulega ametambua mchango mkubwa wa watumishi katika maandalizi ya bajeti hiyo na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa maarifa, weledi na uzalendo. Amehimiza umuhimu wa kuyaendeleza mazingira ya kazi yaliyo na motisha na mshikamano, akisisitiza kuwa viongozi wahakikishe wanaweka mazingira bora ya kazi ikiwemo kuhakikisha wanatoa motisha kwa Watumishi ili kuleta utulivu katika kazi ikiwemo kujenga morali ya kazi na uzalishaji wa tija. Pia amesisitiza Watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na wanakuwa wabunifu katika kazi zao kwa lengo la kuliongezea tija Taifa.

Aidha, amewasihi viongozi wa Taasisi zote zikiwemo TANROADS, TBA, TEMESA, pamoja na bodi za usajili na ujenzi, kuhakikisha usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kujenga uchumi imara kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya akizungumza katika kikao hicho amewapongeza watumishi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika maandalizi ya bajeti. Amehimiza kuendeleza motisha, ubunifu na moyo wa kujituma katika utekelezaji wa majukumu, huku akitoa shukrani kwa Menejimenti ya Wizara kwa ushirikiano mzuri unaoendelea kuiongezea heshima sekta ya ujenzi.

Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Kavishe amempongeza Waziri kwa uongozi wake thabiti na kuahidi kuwa wafanyakazi wapo tayari kuendelea kufanya kazi kwa bidii kama alivyowasihi katika hotuba yake na kuhakikisha kazi zinazofanyika zinakidhi malengo ya Wizara na Taifa kwa ujumla.