Wakala Wa Huduma Ya Ununuzi Serikalini

"Ununuzi Unaozingatia Thamani"

HISTORIA YA WAKALA WA HUDUMA YA UNUNUZI SERIKALINI (GPSA)

Historia ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), inakwenda nyuma zaidi, pale mwaka 1901 Serikali ya Wajerumani ilipoanzisha Bohari Kuu Bagamoyo, mkoani Pwani kwa lengo la kuwezesha huduma ya kununua, kutunza na kusambaza vifaa vilivyokuwa vikihitajika katika shughuli za kila siku Serikalini pamoja na kutunza vyakula vya watumishi wa Kijerumani. Wajerumani walijenga jengo la Bohari Kuu ufukweni eneo la Kaole ambapo ndani yake mlikuwa na ghala lililotumika kuhifadhi vyakula vya watumishi wa Serikali hiyo.

Baadaye, mwaka 1945, baada ya Vita Kuu ya pili ya Dunia Bohari Kuu ilihamishiwa Dar es Salaam ambapo iliongezewa majukumu ya kugomboa mizigo bandarini na kuuza vilainishi na mafuta ya magari. Uhamisho huo ulitokana na sababu za kiutawala kwa kuwa makao makuu ya Wajerumani yalikuwa Bagamoyo, wakati ambapo makao makuu ya Waingereza yalikuja kuwa Dar es Salaam, na ndipo hapo ikaongezewa huduma za Ugomboaji na Uondoshaji mizigo pamoja na huduma ya mafuta ya gari na vilainishi vya mitambo.

Baada ya Vita Kuu ya pili ya Dunia, Bohari Kuu ilihamishiwa Dar es Salaam. Uhamisho huu ulitokana na sababu za Kiutawala kwa kuwa Makao Makuu ya Wajerumani yalikuwa Bagamoyo, wakati Makao Makuu ya Waingereza yalikuja kuwa dar es Salaam, na ndipo ikaongezwa huduma ya Ugomboaji na Uondoshaji Mizigo pamoja na Huduma ya Mafuta ya gari na vilainishi vya mitambo.

Mnamo mwaka 1952, kwa lengo la kuleta ufanisi, Serikali ya Kikoloni ilihamisha jukumu la kutoa vifaa vya ofisi, ambalo hapo awali lilikuwa chini ya Ofisi ya Mchapaji Mkuu wa Serikali, na kulikabidhi kwa Bohari Kuu ya Serikali. Lengo lilikuwa kumruhusu Mchapaji Mkuu wa Serikali kujikita kwenye kazi ya uchapishaji na kuiacha Bohari Kuu ishughulikie masuala ya uhifadhi na usambazaji.

Maghala (Depots) yalianzishwa katika vituo nane vya utawala vya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Morogoro, Kigoma, Arusha, Mwanza na Tabora ili kuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana kote nchini.

Katika miaka iliyofuata, idadi ya maghala hayo ilibaki vile vile hadi wakati wa Uhuru mnamo mwaka 1961, ambapo maghala mapya manne yalifunguliwa huko Kilimanjaro, Dodoma, Mbeya na Lindi. Zaidi ya hayo, Serikali iliamua kuongeza mtaji wa Bohari Kuu kwa kuanzisha mfuko maalum ujulikanao kama Mfuko wa Bohari Kuu ya Serikali wenye mtaji wa Shilingi za Kitanzania milioni 24.6. Mfuko huu ulianzishwa chini ya kifungu cha 17 (3) cha Sheria ya Hazina na Ukaguzi wa Hesabu ya mwaka 1961 (Exchequer and Audit Ordinance of 1961).

Kufikia mwaka 1972, idadi ya maghala ilikuwa imeongezeka kutoka kumi na mawili hadi ishirini. Hii ilifanyika sambamba na uamuzi wa Serikali wa kupeleka madaraka (decentralize) ya utawala katika mikoa. Katika ngazi ya mikoa, Bohari Kuu ya Serikali ilikuwa ikifanya kazi chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa hadi mwaka 1986, ilipohamishiwa Wizara ya Ujenzi. Mnamo mwaka 1980, Bohari Kuu ilirekebishwa ili kuwa Idara ya Ugavi na Huduma ikiongozwa na Mkurugenzi ambaye pia alikuwa na jukumu la ziada la kusimamia maendeleo ya kada ya ugavi na maghala katika utumishi wa umma, jukumu ambalo hapo awali lilikuwa chini ya Hazina.

Kupitishwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004, ambayo kupitia kwayo Wizara, Idara na Wakala (MDAs) waliruhusiwa kununua bidhaa za matumizi ya pamoja kutoka soko huria, ilikuwa hatua nyingine muhimu katika historia ya Idara ya Ugavi na Huduma. Idara hiyo ilipewa jukumu la ziada la kupanga na kusimamia Mikataba Maalum (Framework Contracts) kwa ajili ya bidhaa, kazi, na huduma za matumizi ya pamoja kwa Taasisi zote za Serikali (MDAs).

Majukumu na malengo ya Idara ya Ugavi na Huduma yamebadilishwa ili kuendana na maboresho yanayoendelea ya Serikali na kukabiliana na maendeleo ya kiteknolojia na mabadiliko ya soko. Ili kutoa huduma zake kwa ufanisi na tija, Idara ya Ugavi na Huduma ilirekebishwa kimuundo ili kufanya kazi kama Wakala wa Serikali unaojulikana kama Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).

Kuanzishwa kwa Wakala ni matokeo ya Programu ya Maboresho katika Utumishi wa Umma, yenye lengo la kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma. Kufuatia maboresho haya, iliyokuwa Bohari Kuu ya Serikali ilifutwa, na baadhi ya majukumu yake yalichukuliwa na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA). GPSA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala Na. 30 ya mwaka 1997, kama ilivyorekebishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 235 la tarehe 7 Desemba, 2007. Wakala ulizinduliwa rasmi tarehe 16 Juni, 2008. Wakala una ofisi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na uko chini ya Wizara ya Fedha.