WANAFUNZI WA UNUNUZI NA UGAVI WAHIMIZWA KUJISAJILI KIDIJITALI
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Bodi ya watalaam wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB) iliandaa ziara ya semina ya uhamasishaji juu ya mambo mbalimbali kwa vyuo vinavyotoa kozi ya ununuzi na ugavi nchini.
Ziara hiyo iliyoanza shughuli ya kutembelea vyuo hivyo mwezi May 2025, ilikuwa na malengo ya kuongeza idadi ya watalaam wa sekta ya ununuzi na ugavi waliosajiliwa, kuhimiza wanafunzi wanaohitimu masomo yao kujisajili kwaajili ya mitihani ya kitaaluma pamoja na uanachama.
Viongozi wa PSPTB waliofika katika vyuo vya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Iringa kuzungumza na wanafunzi na watumishi mbalimbali wa vyuo vya ununuzi na ugavi ambapo PSPTB imewataka wanafunzi kuendelea kufuata miongozo, kanuni na sheria iliyowekwa na bodi ili kuwasaidia katika masuala yao ya kitaaluma.
Kwa upande wake Dkt. Juliet Kwashuma Mkufunzi chuo cha Bahari Dar es salaam alisema kuwa Mafunzo yaliyotolewa kupitia ziara hiyo yataendelea kuwaweka wanafunzi karibu na bodi hiyo ili kurahisisha kujifunza na kupata huduma mbalimbali zitolewazo na bodi hiyo.
“Kwa sasa hivi ajira za kada ya ununuzi na ugavi lazima yule anayeajiriwa awe anatambulika na bodi ya ununuzi kwahiyo tunaamini kwamba wanafunzi wetu wameelewa na watakuwa watiifu na elimu hii itawasaidia katika kwenda kulijenga taifa letu.” Amesema Dkt. Kwashuma.
Ziara hiyo iliyolenga pia kuimarisha uhusiano kati ya PSPTB na vyuo vilivyopo chini yake ilifanikiwa kufika katika chuo kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dar es salaam Maritime Institute (DIM), Mwalimu Nyerere Memorial Academy (MNMA), Kilimanjaro Institute of Technology (KITM) pamoja na Chuo cha Utawala wa Biashara (CBE) kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mkoa wa Morogoro maafisa kutoka PSPTB walifika katika chuo kikuu cha Muslim University of Morogoro (MUM) pamoja na chuo kikuu cha Mzumbe ilihali kwa mkoa wa Iringa chuo kikuu cha Mkwawa na Tumaini University of Iringa vilifikiwa na bodi hiyo.
Mbali na mafunzo hayo ya uhamasishaji kufanyika katika vyuo hivyo zaidi ya wanafunzi 1000 wanaosoma masomo ya ununuzi na ugavi kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada na waliosajiliwa walipatiwa mafunzo hayo.
Bodi hiyo imewahimiza zaidi wanafunzi kujisajili kwa njia ya mtandao hususani kuwa mwanachama wa bodi hiyo, usajili wa mitihani ya kitaaluma pamoja na mafunzo mbalimbali ambayo hutolewa na bodi kwa wanachama wake.