Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MFUKO WA MISITU TANZANIA

Jamii

Mfuko wa Misitu Tanzania unatoa ruzuku kwa waombaji wanaotekeleza shughuli zinazochangia maendeleo ya misitu na kuboresha utunzaji wa misitu, uhifadhi na usimamizi wa misitu Tanzania Bara. Vikundi vya kijamii vinaweza kuomba ruzuku ndogo ya kiasi cha fedha kisichozidi shilingi Milioni Kumi (TZS 10,000,000/=) kwa ajili ya miradi ya upandaji miti au ufugaji nyuki. Aidha, vitawasilisha maandiko yaliyoandaliwa kwa kufuata muundo unaotolewa kila mwaka tangazo la kuomba ruzuku linapotangazwa.

Andiko la kuomba ruzuku linatakiwa kuambatana na vielelezo vifuatavyo:

i) Barua ya udhamini kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa na Kata kilipo kikundi;

ii) Barua ya udhamini kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa mradi utakapotekelezwa;

iii) Barua ya udhamini kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri mradi utakapotekelezwa;

iv) Kivuli cha cheti cha usajili wa kikundi kilichothibitishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri kiliposajiliwa kikundi;

v) Muhtasari wa kikao cha wanachama wa kikundi kilichopitisha andiko la mradi uliosainiwa na wanachama wote na kugongwa muhuri wa Afisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa husika;

vi) Uthibitisho wa umiliki wa ardhi (hati miliki au hati miliki ya kimila, mkataba au hati ya mauziano ya ardhi, barua na muhtasari kutoka Serikali ya Kijiji kwa CBO iliyopatiwa ardhi na vijiji), kwa miradi ya upandaji miti;

vii) Kibali cha kuruhusiwa kufanya shughuli za ufugaji nyuki ndani ya misitu ya hifadhi au maeneo mengine yaliyohifadhiwa (kwa miradi ya ufugaji nyuki). Aidha, vikundi vinavyomiliki misitu ya asili na vinaitumia kwa shughuli za ufugaji nyuki vinaweza kuwasilisha uthibitisho wa umiliki wa ardhi na muhtasari wa makubaliano ya wanakikundi yaliyothibitishwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa husika; na

viii) Kwa miradi inayohusisha ununuzi wa vifaa na/au vitendea kazi, waombaji wawasilishe vidadisi bei (quotation);