Upandaji Miti
UTANGULIZI
Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu ambapo hekta takriban milioni 20 ni misitu ya asili kwa ajili ya uzalishaji yaani misitu ya asili inayoruhusiwa kuvunwa kwa utaratibu maalum. Shughuli za uvunaji miti katika misitu ya asili zinafanyika katika misitu inayosimamiwa na Serikali Kuu, misitu iliyochini ya Serikali za Mitaa na misitu iliyopo katika ardhi ya vijiji. Katika kuweka utaratibu mzuri wa uvunaji katika misitu ya asili na kuhakikisha kuwa biashara ya mazao ya misitu inakuwa endelevu, mwaka 2015 Wizara ya Maliasili na Utalii iliandaa “Mwongozo wa Uvunaji Endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu yanayovunwa katika Misitu ya Asili”. Mwongozo huo ulifanyiwa maboresho mwaka 2017 na umeweka utaratibu wa kudhibiti uvunaji na biashara ya mazao yanayovunwa katika misitu ya asili. Kwa mujibu wa mwongozo huo, wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanapaswa kulipa tozo ya asilimia tano (inayojulikana kama “5% tree planting levy”), kwa ajili ya kugharamia shughuli za upandaji miti. Aidha, kila mita moja ya ujazo wa miti inayovunwa katika misitu ya asili inatakiwa kutozwa asilimia tano (5%) ya mrahaba kwa ajili ya kugharamia upandaji miti. Lengo la tozo hiyo ni kuchangia kurejesha uoto wa asili katika maeneo yaliyovunwa na kuongoa maeneo yaliyoharibika kwa kupanda miti.
Mwongozo wa Uvunaji Endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu yanayovunwa katika Misitu ya Asili umeainisha kuwa fedha za tozo ya upandaji miti zinakusanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kuwasilishwa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF). Aidha, Mfuko una jukumu la kutoa (kurejesha) fedha hizo kwa halmashauri ya wilaya iliyokusanya tozo hiyo au Halmashauri nyingine kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za upandaji miti.
Pamoja na kuwepo kwa Mwongozo wa kudhibiti uvunaji na biashara ya mazao yanayovunwa katika misitu ya asili, kumejitokeza changamoto za matumizi na usimamizi wa fedha za tozo ya upandaji miti zinazotolewa kwa halmashauri husika. Baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni fedha za tozo ya upandaji miti kutotumika kwa shughuli za upandaji miti na kukosekana kwa uratibu tozo hiyo. Kufuatia changamoto hizo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), zilisasaini makubaliano (Memorandum of Understanding - MoU) yenye lengo la kuboresha ukusanyaji, utoaji, matumizi, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti. Aidha, Kamati ya kuratibu utekelezaji wa MoU tajwa ambayo ina Wajumbe 5 kutoka MNRT, OR - TAMISEMI, TFS, TaFF na mwakilishi wa wafanyabiashara wa mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu ya asili iliteuliwa ikiwa ni takwa mojawapo la MoU.
Wakati wa utekelezaji wa MoU tajwa, zilibainika changamoto kadhaa ikiwemo ya fedha za tozo ya upandaji miti kutotumika kwa shughuli za upandaji miti. Chimbuko la changamoto hii ni utaratibu unaotumika wa kutoa fedha kwenda kwa Halmashauri zilizokusanya tozo hiyo bila kujali kama kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupandwa miti. Kuendelea kujitokeza kwa changamoto ya matumizi na usimamizi wa tozo ya upandaji miti kumeibua hitaji la kuboresha utaratibu unatumika wa kutoa fedha kwa kuandaa mwongozo ambao utatoa utaratibu mzuri wa ukusanyaji, utoaji, matumizi, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti.
Malengo ya Mwongozo wa Ukusanyaji, utoaji, matumizi, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti
Lengo kuu la Mwongozo
Lengo kuu la mwongozo huu ni kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji, utoaji, matumizi, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti.
Malengo mahususi ya Mwongozo
- Kuboresha utaratibu wa ukusanyaji na utoaji wa fedha za tozo ya upandaji miti;
- Kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha za tozo ya upandaji miti; na
- Kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti na miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha za tozo ya upandaji miti.
Wadau Muhimu wa Mwongozo wa Ukusanyaji, Utoaji, Matumiz, Usimamizi na Ufuatiliaji wa Fedha za Tozo ya Upandaji Miti
Mwongozo huu unalenga wadau wote wanahusika na uchangiaji, ukusanyaji, utoaji, matumizi, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za tozo ya upandaji miti. Wadau ni kama ifautavyo:
- Wafanyabiashara wa mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu ya asili;
- Serikali za vijiji;
- Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji;
- Kamati ya kuratibu tozo ya upandaji miti;
- Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS);
- Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF);
- Kamati za uvunaji za Wilaya;
- Sekretarieti za Mikoa;
- OR – TAMISEMI; na
- Wizara ya Maliasili na Utalii.
UOMBAJI WA FEDHA ZA TOZO YA UPANDAJI MITI
Uombaji wa fedha za tozo ya upandaji miti unafuata utaratibu unaotumiwa na Mfuko wa Misitu Tanzania kwa kuzingatia matakwa ya tangazo la kuwasilisha maandiko ya kuomba ruzuku ruzuku linalotolewa kila mwaka. Waombaji wa fedha za tozo ya upandaji miti watawasilisha maandiko ya miradi ambayo yataandaliwa kwa kufuata muundo unaotolewa kila mwaka tangazo likitolewa. Maombi ya fedha za tozo ya upandaji miti yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya mtandao (online application) kwa kufuata anwani portal.maliasili.go.tz. Baada ya maombi ya fedha za tozo ya upandaji miti kupokelewa, waombaji watajulishwa kuhusu kupokelewa kwa maombi yao kupitia barua itakayoandikwa na Mfuko wa Misitu Tanzania.
UCHAMBUZI WA MAOMBI YA FEDHA ZA TOZO YA UPANDAJI MITI
Maombi ya fedha za tozo ya upandaji miti yatafanyiwa uchambuzi wa awali na Kamati ya kusimamia tozo ya upandaji miti na uchambuzi wa kina utafanywa na Kamati ya Uchambuzi wa maandiko yanayoombwa ruzuku ya TaFF. Taarifa ya uchambuzi wa kina kwa maombi ya fedha za tozo ya upandaji miti itawasilishwa kwa Bodi ya Wadhamini ya TaFF kwa ajili ya uamuzi kuhusu utoaji wa fedha za tozo ya upandaji miti. Wakati wa uchambuzi wa awali, Kamati ya kusimamia tozo ya upandaji miti itapendekeza maandiko ya miradi ya kuomba fedha za tozo ya upandaji miti ambayo yatafanyiwa uchambuzi wa kina na maandiko ambayo hayastahili kufanyiwa uchambuzi wa kina.
MALIPO YA FEDHA ZA TOZO YA UPANDAJI MITI KWA MIRADI ILIYOIDHINISHWA
Baada ya Bodi ya Wadhamini ya TaFF kuidhinisha miradi ambayo itapatiwa fedha za tozo ya upandaji miti, Mfuko wa Misitu Tanzania utawasilisha kwa Kamati ya kusimamia tozo ya upandaji miti taarifa inayoonesha majina ya halmashauri na wadau wengine waliopatiwa fedha za tozo ya upandaji miti na kiasi cha fedha kilichoidhinishwa kwa kila halmashauri au mdau. Aidha, TaFF itawasilisha taarifa inayoonesha hatua zilizofikiwa ya malipo ya fedha za tozo ya upandaji miti baada ya uamuzi wa Bodi. Hatua hizo ni pamoja na kusainiwa kwa mkataba na malipo kufanyika, na iwapo malipo hayakufanyika, TaFF itawasilisha sababu za kutofanyika kwa malipo.
UFUATILIAJI WA FEDHA ZA TOZO YA UPANDAJI MITI NA SHUGHULI ZINAZOTEKELEZWA KWA KUTUMIA FEDHA HIZO.
Kamati ya kusimamia tozo ya upandaji miti itafanya ufuatiliaji wa makusanyo na utoaji wa fedha za tozo ya tozo ya upandaji miti pamoja na shughuli zinazotekelezwa kwa kutumia tozo hiyo. Kamati itafanya kazi hiyo kupitia vikao ambapo taarifa mbalimbali zitawasilishwa. Aidha, Kamati itafanya ziara kwa lengo la kuhakikisha kuwa fedha zitokanazo na tozo ya upandaji miti zinakusanywa na kutolewa ipasavyo, na zinatumika kwa shughuli zilizokusudiwa.