SOKO LA MAZIWA KILIO CHA WAFUGAJI DODOMA
Wakati viwanda vya maziwa nchini vikilalamika kukosa maziwa ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa hali ni tofauti kabisa kwa baadhi ya wafugaji jijini Dodoma ambapo wanakosa soko la kuuzia maziwa yao.
Hayo yamebainishwa na Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa wa Kata ya Nzuguni jijini Dodoma Bw. Ebenezer Nnko alipotembelewa na timu ya Wataalamu toka Bodi ya Maziwa Tanzania Januari 31, 2023 kwa lengo la kujua changamoto mbalimbali anazokumbana nazo katika shughuli zake za ufugaji.
Akizungumza na wataalamu hao, Bw. Nko ameieleza Bodi ya Maziwa Tanzania kuwa changamoto kubwa anayokumbana nayo kwa sasa ni mahali pakupeleka maziwa yake kwani kwa siku anapata lita 150 kiasi kwamba hata akiuza rejareja hawezi kuyamaliza kwa siku moja nay eye bado ni mfugaji mchanga hana vifaa vya kitaalamu vya kuhifadhi maziwa hayo.
"Ninazalisha wastani wa lita 150 kwa siku lakini nakosa pakuyauza, nashukuru kwa kutembelewa na Bodi ya Maziwa Tanzania leo hii huenda changamoto yangu ikapata suluhu." Amesema Bw. Nnko.
Akizungumzia kuhusu changamoto hiyo Kaimu Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu amesema Idara yake itashughulikia na kuhakikisha Mfugaji huyo anapata soko la Maziwa hayo.
"Dodoma tuna viwanda vitatu ambapo viwili vinafanya kazi na kimoja kinatarajia kuanza shughuli zake hivi karibuni, lakini tuna wasindikaji wengi wa maziwa tutawasiliana nao na kuwajulisha ili waweze kuchukua maziwa kutoka kwako." Amesema Bw. Semu.
Kwa upande wake Afisa Uzalishaji Maziwa wa Bodi ya Maziwa Tanzania kwa niaba ya Idara ya Ufundi Maziwa, Bw.Rajilan Shanga amemshauri mfugaji huyo mambo kadhaa ili kuongeza uzalishaji wa maziwa ikiwemo kuzingatia uwiano wa vyakula anavyowapatia mifugo hiyo, kuongeza eneo ili mifugo ipate sehemu ya kupumzika na wanapohitaji kufanya hivyo badala ya kula na kulala katika zizi moja ambalo halina nafasi ya kutosha.
Kuhusu suala la malisho Maafisa hao wamemshauri Bw. Ebenezer kukata majani mengi kwa kipindi hiki na kuhifadhi kwenye ghala lake ili kimsaidie baadae wakati wa ukame.
Bodi ya Maziwa Tanzania inaendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuwatembelea wafugaji, wasindikaji na wafanya biashara wa maziwa kwa ajili ya kuwatambua, kuwasajili na kutatua changamoto zinazowakabili.