Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi iliyoanzishwa Mei 17, 2002 chini ya Sheria ya Wakala Sura 245. Sheria hiyo inatumika pamoja na Agizo la kuanzishwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania lililochapishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 24 la tarehe 14 Februari, 2003 na kuhuishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 595 la tarehe 25 Agosti, 2023. Kuanzishwa kwa Wakala ni moja ya matokeo ya programu ya maboresho ya Sekta ya Umma (“Public Service Reform Program” (PSRP)) ambayo iliitaka Serikali ijikite zaidi katika kuandaa sera zenye kuwezesha kutoa huduma bora kwa Umma na kuleta maendeleo ya kijamii. Wakala wa Majengo Tanzania ulichukua majukumu ya iliyokuwa Idara ya Majengo chini ya Wizara ya Ujenzi.